Na Baraka Mbolembole
BAADA ya kukamilisha usajili wa washambuliaji Emmanuel Martin na kiungo mkabaji raia wa Zambia, Justine Zulu kocha mpya wa kikosi hicho Mzambia, George Lwandamina ataisimamia Yanga katika mchezo wake wa kwanza ‘rasmi’ vs JKT Ruvu ya Pwani siku ya Jumamosi katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Lwandamina anasaidiwa na Watanzania, Juma Mwambusi na kocha wa magolikipa Juma Pondamali huku aliyekuwa kocha wa timu hiyo-mshindi mara mbili mfululizo wa VPL na taji la FA Mholland, Hans van der Pluijm akiwa ‘bosi kubwa’ baada ya kubadilishiwa majukumu na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi klabuni hapo.
WANAENDA KILELENI
Yanga iliifunga 4-0 JKT Ruvu katika mchezo wao wa mwisho kabla ya ligi kusimama mwezi uliopita, bila shaka wataifunga tena timu hiyo inayonolewa na Bakari Shime na kwenda kileleni mwa VPL kwa tofauti ya pointi moja mbele ya Simba itakayocheza na Ndanda FC siku ya Jumapili.
Yanga wana kikosi kipana na chenye muunganiko bora ndiyo maana nasema wataifunga JKT Ruvu na kwenda kileleni mwa msimamo.
Ikumbukwe baada ya kila timu kucheza michezo 13 mabingwa hao watetezi walikuwa nyuma kwa alama 8 dhidi ya vinara Simba SC.
Nadhani ‘nguvu ya historia’ itawasaidia kwa kiasi kikubwa kuifunga JKT Ruvu hapo Kesho.
Historia imekuwa ikiwasaidia sana Yanga katika ushindi wao wa mataji 26 waliyokwisha yatwaa katika ligi kuu huku ‘tabia yao’ ya kutoka chini ya msimamo na kwenda kushinda ubingwa imekuwa ya kipekee. Yanga ilishatengeneza historia ya kutoka chini ya msimamo na kutwaa ubingwa.
UBORA WA SAFU YA MASHAMBULIZI
Hata kabla ya usajili wa Emanuel Martin kutoka JKU kukamilika, Lwandamina tayari alikuwa na ‘hazina’ kubwa ya washambuliaji wafungaji. Mrundi, Amis Tambwe tayari amefunga magoli 7 msimu huu, Mzimbabwe, Donald Ngoma amefunga mara tano sambamba na Mzambia, Obrey Chirwa alifunga magoli matano kati ya 31 ya timu hiyo katika michezo ya mzunguko wa kwanza.
Huku akitaraji ‘kunyanyua’ viwango vya washambuliaji wazawa, Malimi Busungu na Matheo Anthony, kocha huyo wa zamani wa Zesco United ya Zambia amemuongeza mfungaji mpya katika timu Martin Emanuel aliyefanya vizuri wakati akiichezea JKU dhidi ya Yanga katika mchezo wa kirafiki uliochezwa December 10 kwenye uwanja wa Uhuru.
IDARA YA KIUNGO KUIMARIKA ZAIDI
Mnyarwanda, Haruna Niyonzima alikuwa katika kiwango cha juu katika michezo mitano ya mwisho ya mzunguko wa kwanza. Mzimbabwe, Thaban Kamusoko alikuwa na nyakati bora msimu uliopita, kucheza mfululizo pasipo kupumzika kulipunguza kasi yake kutokana na ‘uchovu,’ lakini mwezi mmoja wa mapumziko unaweza kumrudisha katika kiwango chake.
Zulu amesajiliwa ili kucheza katika nafasi ya kiungo-mlinzi. Viungo hawa watatu kutoka ng’ambo ya Tanzania wanaweza kutengeneza safu bora zaidi ya kiungo kuwahi kutokea klabuni hapo miaka ya karibuni.
Wote watatu wanacheza umakini ndiyo silaha yao. Zulu atakuwa akipora mpira, Niyonzima, Kamusoko kwa pamoja watabeba majukumu ya kuichezesha safu ya mashambulizi na kutengeneza nafasi nyingi za upatikanaji wa magoli-kikubwa nao watapaswa kuendelea kujaribu kufunga magoli muhimu kama wanavyofanya siku zote.
Inaonekana wazi, Tambwe na Ngoma watakuwa wakicheza pamoja katika safu yaushambuliaji, huku Niyonzima, Kamusoko na Zulu wakicheza katika kiungo.
Hili likitokea itamaanisha Lwandamina hatakuwa na mchezaji yeyote Mtanzania katika safu ya kiungo na mashambulizi katika kikosi chake cha kwanza.
Watanzania, Said Juma Makapu, Juma Mahadhi, Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya watapaswa kuongeza jitihada katika uwanja wa mazoezi ili kupata nafasi katika safu ya kiungo vinginevyo watasubiri katika benchi na kuwapisha ‘wageni’ kuanza katika kikosi cha kwanza.
Yanga watakuwa na safu bora zaidi ya mashambulizi na kiungo imara. Hii ni sababu nyingine itakayowapeleka kileleni mwa msimamo kwa mara ya kwanza siku ya
Jumamosi hii.
SAFU ILE ILE YA ULINZI
Juma Abdul amepona, Mwinyi Haji, Kelvin Yondan na Mtogo, Vicent Bossou wanataraji kutengeneza ‘ukuta mgumu.’
Yanga imeruhusu magoli 8 katika michezo 15 iliyopita lakini uwepo wa Zulu mbele ya mabeki wa kati utasaidia zaidi safu ya ulinzi kuwa imara. Timu nyingi zilipokuwa zikicheza na Yanga zilitumia ‘mwanya’ wa timu hiyo kukosa kiungo imara-namba 6 kutengeneza nafasi za kufunga magoli.
Zulu atatumika kuua mianya yote ya wapinzani kutengeneza nafasi wakitokea katikati ya uwanja, hivyo basi walinzi wa pembeni nao watapaswa kuzuia krosi zisipigwe kwa wingi katika lango lao na kama watafanikiwa Yanga itakuwa ngumu zaidi kufungika.
KWANINI YANGA HAITASHUKA TENA KILELENI BAADA YA KUPANDA?
Kwanza ratiba iliyo mbele yao. Kama ningekuwa kocha wa timu hiyo ningewaambia uongozi ‘hatupaswi kucheza Mapinduzi Cup’ michuano ya wiki mbili itakayofanyika visiwani Zanzibar kuanzia siku ya mwisho ya mwezi huu hadi Januari 13.
Yanga itakuwa na michuano ya Caf Champions League kuanzia mwezi Februari, pia ni wakati ambao watalazimika kucheza michuano ya FA huku ligi kuu ikiendelea.
Michuano ya Mapinduzi itawachosha zaidi wachezaji ambao wamepumzika kwa muda mfupi sana kulingana na michuano mfululizo waliyoicheza.
Kumbuka baada ya kumalizika kwa msimu wa 2014/15 timu hiyo ilicheza michuano ya Kagame Cup 2015, VPL, Mapinduzi Cup 2016, Champions League, FA, Confederation Cup na kuanza msimu huu wa VPL pasipo kupumzika.
Kama Yanga haitacheza Mapinduzi Cup 2017 watazifunga JKT Ruvu, African Lyon, Ndanda FC (michezo yote hii wakicheza uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam), Majimaji FC (Songea) na Mwadui FC ambao watasafiri kuja Dar.
Ushindi katika michezo hii mitano unaweza kupatikana bila shaka na wapinzani wao watakuwa wakihangaika nje ya Dar es Salaam kusaka ushindi.