Na Baraka Mbolembole
UNAMKUMBUKA, Wazir Mahadhi ‘Mendieta’? Kiungo maridadi sana miaka ya mwanzoni mwa 2000. Upande wangu nakumbuka mengi sana mazuri kuhusu kiungo huyo namba 6 wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania na vilabu vya Coastal Union ya Tanga, Yanga SC na Moro United.
Katika moja ya stori zilizokuwa zikizua mabishano yasiyo na mwisho, ni nani alikuwa mchezaji bora kati ya Mahadhi na aliyekuwa nahodha wa Simba SC, Suleimani Matola. Katika timu ya Taifa mwaka 2001 wachezaji hao wote wawili walikuwa kikosini na mara nyingi makocha wa Stars walikuwa wakimuanzisha Mahadhi.
Mfano wakati wa michuano ya Castle Cup 2001 ambayo Taifa Stars ilitwaa ubingwa jijini Mwanza, Mahadhi alianza katika kikosi cha kwanza katika game ya fainali vs Kenya, lakini alikuja kuumia dakika ya 6 na nafasi yake ikachukuliwa na Matola ambaye aliisaidia Stars kushinda 3-1.
Kuumia mara kwa mara kwa kiungo huyo kulipelekea baadhi ya mashabiki wa Simba kusema ‘fundi mpira huyo alikuwa na laana ‘ ya marehemu baba yake ambaye alipata kuwa golikipa bora ndani ya kikosi cha Simba miaka ya nyuma.
Nimemkumbuka Mahadhi mara baada ya kumsikiliza siku ya Ijumaa katika mahojiano yake na mtangazaji wa Clouds FM, Mbwiga Mbwiguke katika kipindi cha Sports Extra. Mahadhi alielezea namna alivyopata wakati mgumu kuchagua timu ya kujiunga nayo mwaka 2000 kati ya vigogo Yanga na Simba akitokea Coastal Union.
Hivi ndivyo Yanga ilivyomsaini Wazir Mahadhi ‘Mendieta’ kutokea Coastal Union
“Wakati huo nilikuwa nimechaguliwa timu ya Taifa ya vijana U20-Ngorongoro Heroes. Tulienda kucheza mechi huko Msumbiji, sasa wakati tunarudi nyumbani, sina hili wala lile kumbe viongozi wa Simba na Yanga walikuwa tayari wamenifuata Air Port. Wote wanataka saini yangu.”
“Simba walikuja marehemu Juma Salum na Kassim Dewji, huku Yanga nao wakiwa pembeni, Abass Tarimba na Francis Kifukwe. Simba wapo huku na upande mwingine Yanga. Sasa Yanga wamekuja na Bi. Mkubwa (mama yake mzazi,) sasa utaenda wapi ndugu yangu. Ilibidi niende kwa Bi. Mkubwa.”
“Kufika upande aliokuwepo Bi. Mkubwa nikaingizwa ndani ya gari nikapelekwa katika hotel moja kwenda kusaini, sijui Masaki, siikumbuki. Nikala ‘mpunga wangu’ (pesa ya usajili). Nikarudi nyumbani nikamuuliza Bi. Mkubwa ‘wewe umefikaje pale?’ Akaniambia ‘mimi wamenifuata nyumbani (viongozi wa Yanga), wamenipa pesa ndio nikaja.”
“Kwa hiyo na Bi. Mkubwa naye walimdakisha. Tarimba ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili. Hapo hutoki, hata uwe wapi,” anamaliza kusimulia Mahadhi.