Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Yanga SC imekamilisha usajili wa mshambulizi Paul Nonga kutoka timu ya Mwadui FC ya Shinyanga. Wengi wameshangaa kitendo cha mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Bara kumsaini, Nonga kwa kuwa tayari wana washambulizi wasiopungua watano katika kikosi chao.
Mrundi, Amis Tambwe, Mzimbabwe, Donald Ngoma, Malimi Busungu, Matteo Anthony huku pia viungo washambuliaji, Simon Msuva na Deus Kaseke wakiwepo kikosini. JKT Mgambo 0-0 Yanga SC Mechi hii ilikuwa ya kwanza msimu huu kwa Yanga kumaliza dakika 90 pasipo kufunga goli. Kaseke, Msuva, Matteo na Busungu wote walicheza katika mchezo huo wa Jumamosi iliyopita ambao washambuliaji hao walipoteza nafasi nyingi za kufunga magoli.
Mashabiki wamekuwa wakihoji na kuchukulia kitendo cha kumsaini Nonga ni sawa na kummaliza mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za JKT Oljoro na Mbeya City lakini upande wangu naamini Yanga ilipaswa kumsaini Nonga hata kabla ya mchezaji huyo kujiunga na Mwadui FC.
Nonga ni mchezaji wa mechi kubwa na amedhihirisha hilo katika misimu yake miwili aliyochezea City. Msimu huu amefanikiwa kufunga magoli matano, mawili akifunga katika mchezo wa mahasimu wa Mkoa wa Shinyanga (Stand United 0-2 Mwadui FC), pia goli lake la ‘video’ dhidi ya Yanga katika sare ya Mwadui FC 2-2 Yanga bila shaka lilimshawishi kwa kiasi kikubwa mkufunzi wa Yanga Hans Van der Pluijm kupendekeza kusajiliwa kwake Yanga katika dirisha dogo la usajili lililofungwa usiku wa kuamkia Jumatano hii.
Nonga anaweza kuibeba Yanga ikiwa katika wakati mgumu kwa kuwa anaweza kuamua matokeo yasiyotarajiwa kwa uwezo wake wa kufunga magoli ya mbali kwa kiki zake za ufundi. Wakati, Hamis Kiiza alikuwa akicheza kwa kuhaha eneo lote la mashambulizi na kufunga magoli yasiyotarajiwa ambayo yaliibeba sana Yanga katika gemu ngumu, Nonga ni mtu anayependelea kusimama katika safu ya ushambuliaji wa kati na kudhibiti mipira yote inayoelekezwa kwake.
Ana nguvu na umbo ambalo linamsaidia kuongeza uwezo wake wa kumiliki mpira, ana uwezo mzuri wa kutoa pasi za hatari kwa wakati mwafaka na hilo ni jambo ambalo pengine halikuwepo katika safu ya mashambulizi ya Yanga.
Ngoma ndiye kinara wa ufungaji Yanga (amefunga magoli 8) Tambwe anafuatia akiwa na magoli matano lakini mshambulizi huyo wa timu ya taifa ya Burundi hajafunga goli lolote tangu Oktoba, Msuva ambaye ni ‘mtetezi’ wa tuzo ya ufungaji bora amefunga mabao matatu msimu huu, Busungu amefunga magoli mawili wakati Kaseke amefanikiwa kufunga kwa mara ya kwanza tangu aliposajiliwa Yanga katika mchezo wa mzunguko wa tisa dhidi ya Kagera Sugar.
Watano hao wamefunga jumla ya magoli 19 katika mechi kumi msimu huu. Ni idadi nzuri ya magoli lakini kulingana na michuano ijayo ya klabu bingwa Afrika 2016, nafikiri Yanga walihitaji nyongeza zaidi ya mfungaji. Nonga ni mtu sahihi, pia kama Mniger, Diego atakuwa vile anavyotarajiwa bila shaka usajili wa wawili hao utakuwa na maana kubwa katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa mwaka ujao.
Sina shaka kuhusu nafasi ya Nonga kucheza katika timu ya Yanga ikiwa hatokumbwa na majeraha. Niliwahi kuzungumza nae kwa kirefu ni mchezaji ambaye anajiamini, ana nguvu za kuweza kumsaidia kupambana na beki wa aina yeyote, ni mchezaji mwenye nidhamu na uvumilivu. Amepevuka hasa, kiumri na kiuchezaji. Hakika Yanga ilimuhitaji mshambulizi huyu.
Nakumba aliniambia yu karibu kuachana na mpira wa ushindani ndani ya misimu mitatu ijayo na kurejea kufanya kazi aliyoisomea (mambo ya madini) Yanga wamepatia sana kumsaini Nonga mchezaji ambaye hayuko tayari kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania kwa sababu ya ubinafsi ambao anasema amewahi kuushuhudia wakati alipoitwa kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 2013.
Sasa ni jukumu la Nonga mwenyewe kujituma ili kupambana kuingia timu ya kwanza mbele ya Ngoma, Tambwe. Yanga wameongeza mabao na ubunifu katika safu yao ya mashambulizi. Paul Nonga, Ni usajili ‘bab-kubwa,’ Yanga SC ilihitaji mtu wa mechi kubwa.