Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

KILICHOANDIKWA TANZANIA, KIKACHAPWA ABUJA KIKASOMWA TENA TANZANIA

$
0
0
Samatta akiwa ameishikilia tuzo yake vizuri kutoa nafasi kwa waandishi kupiga picha za kumbukumbu
Samatta akiwa ameishikilia tuzo yake vizuri kutoa nafasi kwa waandishi kupiga picha za kumbukumbu

JANA ilikuwepo ndiyo, lakini inasimama kuwa ni kumbukumbu yetu ya leo huku kesho ikiwa ni ndoto yetu ya leo kwani hatujui kipi hasa kitatokea. Tazama mshale wako wa saa, tazama kalenda yako kisha shika paji lako la uso, na utazame juu, utagundua kuwa hata mwaka 2016 umeanza kwenda kwa kasi sana.

Mawazo na fikra hukwambia katika lipi la kukumbukwa daima. Kila chombo cha habari Tanzania kimetawaliwa na habari za kijana mwenye ladha ya kipekee katika miguu yake, Mbwana Samatta.

Kijana aliyeshinda tuzo tuliyozea kumuona Mohamed Aboutrika akiikumbatia, tuzo ambayo kama tukiwa na nia ya dhati ya kuendeleza soka letu basi ni msukumo tosha kwa wasimamizi na wanamichezo.

Pengine inawezekana aliondoka akiwa na upweke kiasi kwa kuwa wengi waliamini nafasi yake ilikuwa finyu kushinda tuzo hii. Kuanzia katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere mpaka Abuja, Samatta alikuwa na timu ya watu wanne pekee.

Yeye Samatta, mchambuzi na mkereketwa wa masuala ya kimichezo Shaffih Dauda, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa na mtu ambaye kasababisha picha na video za Samatta zifikie mboni ya kila Mtanzania kwa usahihi zaidi, mpiga picha na mtayarishaji Raymond Charles.

Mbwana Samatta (katikati) akiwa sambamba na Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine (kulia) pamoja na mwandishi na mchambuzi wa michezo wa Clouds Media Group na shaffihdauda.co.tz
Mbwana Samatta (katikati) akiwa sambamba na Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine (kulia) pamoja na mwandishi na mchambuzi wa michezo wa Clouds Media Group na shaffihdauda.co.tz

Ndiyo, Samata akiwa katika muonekano nadhifu, kichwa kilichotulia na mawazo chanya alipanda ngazi za ndege akiiacha ardhi ya Tanzania akiwa na ndoto ya kesho ambayo hakujua kama itatimia lakini bado aliamini. Pengine macho yake yaling’ara huku masikio yake yakitanuka zaidi alipofika Addis Ababa pale Ethiopia alipokutana na mchezaji mwenzake Robert Kidiaba ambaye wanacheza wote TP Mazembe.

Sura zao zilionesha sasa kuamini walikuwa katika kipindi cha kuandika historia na kumbukumbu ambayo kining’ina wangu ataikuta. Abuja ilee ambapo Issa Hayatou ndiko aliamua tuzo zitolewe Samatta na wenzie wakatua majira ya saa 8:00 mchana, Januari 6, mwaka huu.

Watanzania tumeumbwa na ukarimu na upendo. Ubalozi haukuwa nyuma kumuagiza ofisa wake, Elias Mwandobo kuja kuhakikisha kuwa begi la Samatta lililokuwa na suti na bendera ya taifa linafika salama katika hoteli ya maraha ya Hilton. Gari lililoandaliwa na CAF hiloo, likaondoka Airport kuelekea Abuja mjini umbali wa takribani kilomita 50.

Haukuwa usiku mwepesi, Shaffih alitaka kukusanya habari zenye kujitosheleza, Mwesigwa alipaswa kuhakikisha kijana yupo sawa, Raymond akinasa kila tukio na Samatta akiwa kwenye dimbwi la mawazo.

Ukienda ugenini basi usimsahau aliyekupokea, huo ni ustaarabu wa kiafrika. Samatta na wenzie wakaelekea ubalozini, wakaenda kupata japo kahawa itakayoambatana na salamu za kutakiana kheri maana hata pale kulikuwepo kofia ya mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli.

Baada ya ubalozini lilikuwa jukumu la hawa ndugu watatu kumrejesha Samata mapumzikoni huku wao wakiendelea kufanya yaliyokuwa yanahitajika.

Tuzo zilizomtoa Pierre Emerick Aubameyang Ujerumani na Yaya Toure pale Uingereza. Katika kufuatilia maandalizi ndipo jicho la washenga hawa wa Samatta lilipotua kwenye picha iliyoonyesha kuwa Samatta alikuwa kaingia kwenye 1st eleven ya Afrika. Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza wa Samatta.

4

Ilikuwa ni taarifa ambayo Watanzania ndio walikuwa wa kwanza kuipata. Hata Toure hakuijua kabla ya Mwesigwa. Taarifa hiyo ilipopenya kwenye ngoma za masikio ya Samatta iliamsha tabasamu kwake.

Baada ya muda mshale wa saa uliashiria kuwa ulikuwa muda sahihi wa kuanza kujiandaa na kilichowapeleka kule. Ilikuwa jukumu la Shaffih kuhakikisha suti nadhifu inakaa vyema mwilini kwa Samatta huku straika huyo naye akihakikisha kuwa koti la Shaffih halina hitilafu yoyote.

Samatta hakuchelewa kuzisogelea ngazi, mahala ambapo aliweza kukutana na mtu ambaye wote wananyoa nywele zao za pembeni, mshambuliaji hatari wa Borussia Dortmund,  Aubameyang. Kabla kope hazijafunika macho yake kwa sekunde moja kupisha kijiupepo maridadi kipite akatokea Kiungo wa Manchester City, Toure.

Kwa kipindi hicho Samatta alikuwa katika mnara wa kipekee ambao malaika walisubiri akianguka wamwokoe. Ulikuwa ni muda sahihi wa picha za kumbukumbu.

Tukio la kukumbukwa kwa kila Mtanzania ilikuwa muda ambao Samatta anachukua tuzo Ile. Hakuna aliyejali wakati jina lake linatajwa kwani ingeweza kuwa makosa kama yale aliyofanya Steve Harvey kwa kumtangaza Miss Universe wa dunia kimakosa kisha taji likaenda kwa mtu tofauti.

samagoal

Baada ya utoaji wa tuzo kwa washindi, sasa wote wakaelekea kwenye mahojiano maalumu na waandishi ambayo hayakwenda hewani. Akarudi zake chumbani, akaweka tuzo yake kitandani, akajifunika bendera inayomwakilisha kila Mtanzania akacheka, akatabasamu mpaka usingizi ulipomchukua.

Screen Shot 2016-01-08 at 8.00.47 AM

Jua lilichomoza wakati ambao Samatta yupo kakumbatia tuzo yake. Muda huo ubalozi ulionekana kuwa jirani kuliko kawaida. Tuzo ikapelekwa pale, mheshimiwa Daniel Olenjolai, balozi wa Tanzania nchini Nigeria hakusita kutoa pongezi zake na pia akaongeza na nasaha zake ambazo hapana shaka zilichana ngoma za masikio ya nyota huyo.

Safari ya Dar ndiyo ikawa imeiva rasmi. Kila jema kwa wakati huu liligeuka kuwa baraka kwa Samatta na kama kuna baya ambalo lingejitokeza lingekuwa utukufu pia.

Screen Shot 2016-01-09 at 8.35.01 PM

Hongera sana Samatta, safari ya Dar mpaka Abuja haikuwa nyepesi lakini ulichorudi nacho katika Uwanja wa Julius Kambarage Nyerere ni ushujaa. Wakati huu ambao kila kitu hata kifungua kinywa cha bondia Floyd Mayweather kinahifadhiwa mtandaoni wewe utadumu kwenye kumbukumbu.

Bahati nzuri hata kitabu cha historia hii utaandikwa kwa maandishi makuu. Mtanzania wa kwanza kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika wa Ndani. Unataka nini zaidi, waliokuona wajione kuwa ni wenye bahati sana.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>