
Na Abubakar Khatib ‘Kisandu’, Zanzibar
Timu ya mabaharia ya KMKM inayoshiriki ligi kuu soka visiwani Zanzibar, imethibitisha rasmi kumsajili mlinzi wa kushoto kinda kutoka timu ya Muembe Beni United ambae anaitwa Adam Abdallah na watu wengi humwita ‘BAGAWA’I wakimfananisha na mlinzi wa kushoto wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Yanga Mwinyi Haji Ngwali kwa alivyofanana uchezaji wake na mlinzi huyo.
Mtandao huu tumeongea na kocha Ali Bushir wa KMKM na akithibitisha kumsajili kinda huyo katika dirisha hili dogo la usajili la ligi kuu soka Zanzibar huku kocha huyo akiamini mtoto huyo mwenye miaka 16 atamshinda Mwinyi wa Yanga kwa mafanikio.
“Ni kweli nimemsajili huyu kijana Adam na kwasasa ni mchezaji rasmi wa KMKM, huyu kijana ana kipaji sana na naamini atafika mbali mana yupo kama Mwinyi wa Yanga”, alisema Bushir.
Hatukuishia hapo tukapiga hodi moja kwa moja mpaka kwenye klabu ya Muembe Beni United inayoshiriki ligi za madaraja ya vijana Wilaya ya Mjini na tukazungumza na kocha wa timu hiyo Suleiman Hamid (Mzee Ole) na kuthibitisha kuwa kweli wamemalizana na KMKM kuhusu mchezaji wao ambaye ni BAGAWAI two.
“Ni kweli leo tumemalizana na KMKM kuhusu Adam, naamini huko alipoenda atafanya vizuri maana kocha Bushir anajua kukuza vipaji”, alisema Mzee Ole.
Tukamtafuta mchezaji mwenyewe Adam Abdallah ambaye leo rasmi KMKM wamemsajili huku akifurahi kucheza timu hiyo na amesema kuwa atapambana katika klabu ya KMKM kwenye ligi kuu soka ya zanzibar.
“Nimefurahi kusajiliwa na KMKM na nitaweza kucheza nikipewa nafasi mana Muharami wa Black Sailors ameweza na mimi ntaweza, Kocha Bushir ameniona kwenye timu yangu ndiyo kanisajili, nimefurahi kusajiliwa KMKM pia nawashukuru makocha wangu akiwemo Vigema, Mzee Ole na Kocha Theo maana wote wamenisaidia”, lisema BAGAWAI TWO.