Ukimsifia anayekimbia usiache kumsifia anayemkimbiza, sasahivi mambo yamekuwa matamu kwenye mchuano wa kuwania ufungaji bora kwenye ligi ya Vodacom Tanzania bara kwasababu mbiyo zimepamba moto hasa wakati huu ligi inapoelekea ukingoni.
Jeremia Juma Mgunda ndiye mzawa amabye anawafukuzia wafungaji wanaoongoza mbiyo za ufungaji bora kwenye ligi ambao ni Amis Tambwe wa Yanga na Hamisi Kiiza wa Simba wenye magoli 14 kila mmoja huku Mgunda yeye akiwa na magoli 10.
Mgunda ni mchezaji ambaye ametokea Lipuli moja kwa moja na kujiunga na Tanzania Prisons ikiwa ndiyo timu yake ya kwanza kucheza kwenye ligi kuu Tanzania bara aliisaidia timu yake kupata sare ikiwa mkoani Mbeya dhidi ya Yanga Jumatano ya wiki hii alipofunga bao moja kwenye sare ya magoli 2-2 kwenye mchezo huo.
Yahaya Mohamed amepiga story na Mgunda na kufanya naye mahojiano maalum kujua mengi zaidi kuhusu mchezaji huyo ambayo watu wengi walikuwa hawafahamu mengi kuhusu yeye.
Shaffihdauda.co.tz: Kumekuwa na mkanganyiko wa magoli ambayo umefunga kwenye ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, mpaka sasahivi umeshafunga magoli mangapi?
Mgunda: Kwasasa nina magoli 10 lakini kwingine wanaandika 7 wengine 9.
Shaffihdauda.co.tz: Unaweza ukazikumbuka timu ambazo ulifunga magoli hayo?
Mgunda: Azam nilifunga goli moja, Tabora kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar nilifunga magoli mawili, mechi dhidi ya Majimaji nilifunga magoli mawili, Ndanda nilifunga magoli mawili Mwanza dhidi ya Toto nilifunga goli moja na ile ya Yanga. Kuna game nyingine hapa katikati nilifunga lakini sikumbuki vizuri.
Shaffihdauda.co.tz: Unadhani kwa nini rekodi zako haziko sawa kwenye mitandao mbalimbali wanapoandika idadi ya magoli yako?
Mgunda: Nadhani ni wao wenyewe tu ufatiliaji wao wa mechi za ligi ndiyo unasababisha wasiwe na takwimu sahihi.
Shaffihdauda.co.tz: Kabla ya kujiunga na Tanzania Prisons ulikuwa unacheza kwenye timu gani?
Mgunda: Kabla ya kuja Prisons nilikuwa Lipuli.
Shaffihdauda.co.tz: Ulishawahi kucheza timu yoyote ya ligi kuu kabla ya Tanzania Prisons ?
Mgunda: Hapana sijawahi, nilicheza tu hapohapo Lipuli U17 baadaye nikacheza timu ya mkoa ndiyo wakaniona Prisons baada ya kutupia kwenye mechi dhidi ya Manyara ndiyo wakaniona.
Shaffihdauda.co.tz: Jina lako kamili ni Jeremia Juma Mgunda, unauhusiano wowote na mchezaji wa zamani wa Coastal Union Juma Mgunda ambaye kwasasa ni kocha ?
Mgunda: Hapana sina uhusiano naye ila majina yanafanana tu.
Ukizungumzia wachezaji ambao wako kwenye kiwango cha juu kwa siku za hivi karibuni basi huwezi kuliacha pembeni jiana la Jeremia Juma Mgunda kutokana na mambo ambayo amekuwa akiyafanya uwanjani akiwa na timu yake ya Tanzania Prisons ikiwa ni pamoja na kutupia wavuni.