Katika msimu ambao Simba SC ilishinda ubingwa wake wa mwisho wa ligi kuu Tanzania Bara (2011/12) mambo mengi ya kupendeza yalitokea kwa msimu mzima. Katika michuano ya kimataifa wakiwa wawakilishi wa Tanzania bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Walifanya vizuri kiasi hadi kufika hatua ya 16 ambayo iliwahusisha pia washindwa 8 waliotolewa katika ligi ya mabingwa. Kwa maana hiyo Simba ilikuwa ni miongoni mwa timu 8 bora za michuano ya shirikisho na ‘nusura’ wafuzu kwa hatua ya nane bora kablaya kutolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti na Al-Shandy ya Sudan.
Ulikuwa ni msimu mzuri kwa klabu hiyo pengine zaidi ya ule waliomaliza pasipo kupoteza mchezo wowote ( 2009/10). Hakika ilikuwa ni timu kali iliyokuwa imekusanya wachezaji wazoefu waliochanganyika na vijana waliokuwa na vipaji vya hali ya juu.
Kuelekea mchezo wao wa mwisho wa msimu, 7 Mei, 2012 niliandika wazi katika gazeti la Dimba kwamba wapinzani wao Yanga walikuwa wanakwenda kukutana na kipigo kikubwa. Kwani nilisema vile? Simba ilikuwa timamu kimwili na kiakili kwa msimu mzima na walikuwa na kikosi bora ndani ya uwanja kuliko Yanga.
Shomari Kapombe ndiyo alikuwa ‘moto’ katika beki 2, Kelvin Yondan, Juma Nyosso na nahodha Juma Kaseja waliunda ‘ngome’ kabambe, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango (Mungu amrehemu) walitengeneza safu moja ya kuvutia katikati ya uwanja. Felix Sunzu, Salum Machaku na Emmanuel Okwi walikuwa ‘balaa’ katika safu ya mashambulizi.
Nyota hao na namna walivyozitesa ES Setif ya Algeria na Shandy katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sababu ambayo ilinifanya niseme Yanga walikuwa wakienda kukutana na kipigo kikubwa. Ilikuwaje? Walipigwa 5-0 na mara baada ya goli la tano la Simba kuna matukio mawili yalinivutia.
Ubora wa Simba katika kumiliki mpira, kupasiana na kutengeneza nafasi kwa haraka wakati wakishambulia ilikuwa sababu ya kuifunga Yanga 5-0. Timu ilikuwa imeundwa kumtegemea marehemu Mafisango ambaye alikuwa na maamuzi ya haraka na sahihi wakati wa kushambulia.
Pasi zake ndefu za kwenda mbele zilikuwa sahihi na zilifika kwa walengwa. Mafisango alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi zote tano za nyuma (namba 2, 3, 4, 5 na 6) lakini upande wangu nilipendezwa naye na kumuona kiungo maridadi sana katika upigaji wa pasi za mwisho. Nilimchukulia kama namba 8 aliyekamilika.
Alijua kujilinda na kuilinda timu yake pale inapokuwa katika presha. Kitu cha ziada katika timu nyingi bingwa kama hazina wafungaji wawili wa uhakika, basi ni lazima zitakuwa na kiungo mfungaji wa magoli muhimu katika timu.
Mafisango alifunga jumla ya magoli 11 kwa msimu mzima. Ilikuwa idadi ya juu ya magoli katika timu yake mbele ya washambuliaji, Sunzu na Okwi.
Nakumbuka wakati Simba imetangaza kuwa itamuacha Mafisango katika msafara wao wa Algeria katika mechi ya marejeano na Setif niliwaambia kuwa ‘ni kamari mbaya wameicheza’ licha ya kuwa na ushindiwa 2-0 nilisema watatolewa katika michuano kama hawatabadilisha uamuzi wao wa kumuacha Mafisango.
Nilisema pia watafuzu kwa hatua inayofuata kama tu wangemchukua mchezaji huyo wa zamani wa Rwanda aliyepoteza maisha kutokana na ajali ya gari Mei 17, 2012 siku kumi tangu afunge goli la mwisho la msimu wa 2011/12 kwa timu yake ya Simba.
Katika pasi ambazo ni nadra kuziona ni ile aliyompasia, Okwi dakika ya 90+3 katika mchezo wa marejeano ugenini dhidi ya Setif. Simba ilikuwa pungufu tangu mwanzo wa mchezo baada ya Nyosso kuondoshwa uwanjani kwa kadi nyekundu ya kizembe, matokeo yalikuwa Setif 3-0 Simba na yalikuwa yakiwatupa nje ya michuano ‘Wekundu wa Msimbazi.’
Baada ya kucheza kama mlinzi wa kati kwa muda mwingi kufuatia kutolewa kwa Nyosso, dakika za mwisho mwisho nilimuona kocha Milovan Curkovic akimpa nafasi mlinzi Victor Costa ‘Nyumba’ hilo lilimpa nafasi Mafisango kusogea katika kiungo.
Nilimwambia rafiki yangu tuliyekuwa tukitazama naye gemu ile, ” Simba atafuzu sasa, lazima Mafisango atafanya kitu na tutapata goli la ugenini.” baada ya dakika kadhaa, Mafisango aliuchukua mpira uliokuwa umeanzia nyuma, akakimbia nao kwa kasi akiwahi muda, akili alifahamu kuwkuwa lile lilikuwa jaribio lao la mwisho katika mechi kwani mwamuzi aliongeza dakika 4 tu.
Kwa uhakika akaupunguza uwanja, huku macho yakiwa juu akawa anamtafuta Okwi na Mganda huyo kwa kasi licha ya kwamba alikuwa amechoka, akaikimbilia pasi ndefu maridadi iliyowekwa njiani na Mafisango.
Daah! Kilichotokea, si rahisi kusimulia namna Okwi alivyofunga goli lile kali katika dakika ya mwisho ya mchezo baada ya shambulizi timilifu lililofanywa na mchezaji mmoja tu Mafisango huku timu ikiwa pungufu.
Kufungwa 3-0 na Shandy katika dakika 45 za mwisho kisha kupoteza mechi katika hatua ya mikwaju ya penalti hadi sasa naamini kuwa mechi ile ni muendelezo wa michezo muhimu ya kimataifa ‘inayouzwa’ na klabu masikini kwa zile tajiri barani Afrika.
Ile ilikuwa Simba hatari na Yanga walifungwa huku wanacheka. Walikuwa wakimcheka mwenyekiti wao Nchunga ambaye alijinasibu kuwa ni kiboko ya Simba. Goli la 5 la Simba lilipotinga nyavuni, mfungaji wa goli hilo, Mafisango alikimbia katika moja ya kona za uwanja wa Taifa na kushangilia kwa stahili ya kucheza stahili fulani hivi ya muziki huku mkono wake mmoja akiuchezesha juu kama mtu aliyekuwa akiwaambia mashabiki wa Yanga kuwa ‘tumewakata mkono.
‘Mashabiki wengi wa Yanga waliokuwa wamekwisha ondoka uwanjani hasa baada ya golikipa wa Simba, Juma Kaseja kuifungia timu yake goli la tatu. Wale mashabiki wavumilivu walibaki na baada ya kufungwa goli la tano walianza kupaza sauti’ “Hizo tano zinatosha. Hatutaki aibu zaidi. Hatutaki yajirudie ya 6-0”.
Hawakuwa wakitania na kama wachezaji wa Yanga wasingecheza kwa nguvu dakika kumi za mwisho kuzuia goli la 6 basi ingetokea vurugu kati yao na mashabiki wa timu yao.
Tano zitarudi tena Jumamosi. Atapigwa nani? Naitafuta kwanza namba 30 ya Simba kwa mwaka wa nne sasa, nikiipata nitajua 5 zinarudi wapi. ‘Rest In Peace, Patrick Mutesa Mafisango’ wewe ndiye uliyeondoka na ‘number30’ ya Simba.