Na Baraka Mbolembole
Ligi kuu Tanzania Bara inaelekea mzunguko wake wa 21 mwishoni mwa wiki hii kwa timu zote 16 kupambana katika kusaka alama tatu muhimu. Hadi sasa si rahisi kufahamu ni timu gani inaweza kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu lakini timu za Yanga SC, Azam FC na Simba SC mojawapo inaweza kushinda ubingwa huo.
Vita nyingine ni ile ya kuwania nafasi ya nne hadi ile ya 6 (nafasi ambayo huzifanya timu kuingia katika bodi ya ligi).
Vita kali nyingine msimu huu inataraji kuwepo katika eneo la kushuka daraja. JKT Ruvu, African Sports, na Coastal Union zinaweza kushuka endapo hazitafanya jihada kujinasua katika nafasi walizopo sasa (nafasi ya 16 kwa JKT Ruvu, nafasi ya 15 kwa Sports na nafasi ya 16 kwa Coastal kabla ya mechi za wikendi hii).
Hapa nakuletea uchambuzi na mtazamo wangu kuhusu VPL ilivyo na inavyoweza kuwa baada ya gemu za Jumamosi na Jumapili hii.
AZAM FC v YANGA
Hii pia ni mechi ngumu na itafuatiliwa sana kwa kuwa inazikutanisha timu mbili za juu na katika msimu wa nane wa uwepo wa Azam FC katika ligi mechi baina yao imekuwa ngumu na kadri miaka inavyozidi kusonga mbele pambano la Azam FC v Yanga SC linazidi kuwa na mvuto mkubwa
Kikubwa kinachofanya mechi kati ya timu hizi kuwavutia wengi ni ushindani wa ndani ya uwanja. Azam itakuwa wenyeji katika mchezo wa Jumapili hii na wanashika nafasi ya pili nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi moja lakini wana mchezo mmoja wa kiporo (dhidi ya Stand United)
Yanga ambao waliifunga Simba SC na kurejea kileleni katika mchezo wao wa mwisho inahitaji ushindi pia ili kutengeneza gap la pointi nne dhidi ya wapinzani wao hao wakubwa katika mbio za ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo sasa.
Ikiwa na pointi 46 kileleni mwa msimamo na mchezo mmoja zaidi ya Azam wenye pointi 45 bila shaka watakuwa wakitambua wazi kuwa kushindwa kushinda itakuwa ni sawa na kuwapa ‘mwanya’ wapinzani wao hao.
Mechi 15 zilizopita baina ya timu hizo katika VPL zimeshindwa kumtoa ‘mbabe,’ kila timu imefanikiwa kushinda mara 5 na michezo mingine mitano ikimalizika kwa matokeo ya sare. Mechi ya kwanza msimu huu timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana goli 1-1.
Timu hizo zilikutana katika robo fainali ya michuano ya CECAFA Kagame Cup mwezi Julai, 2015 na hadi muda wa kawaida wa mchezo unamalizika matokeo yalikuwa 0-0, Yanga wakapoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti na kuondolewa katika michuano ambayo Azam FC walishinda ubingwa.
Zikakutana tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Septemba, 2015 na kwa mara nyingine dakika 90 zilimalizika kwa matokeo ya 0-0, safari hii Yanga walishinda katika changamoto ya mikwaju ya penalty.
Baada ya sare ya 1-1 katika VPL mwezi Disemba, 2015 timu hizo zilikutana tena Januari hii katika hatua ya makundi ya michuano ya Mapinduzi Cup huko Visiwani Zanzibar na mechi hiyo iliyokuwa na ubabe mwingi ilimalizika kwa sare ya kufungana 1-1.
Ukitazama rekodi hiyo utagundua kuwa ndani ya miezi takribani 7 zimekutana mara nne na hakuna timu iliyokubali kupoteza mchezo ndani ya dakika 90.
Nahodha wa Azam, John Bocco ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu katika gemu ya Mapinduzi amekuwa na rekodi ya kipekee ya kuifunga Yanga kuliko mchezaji ye yote yule ataongoza tena safu ya mashambulizi ya kikosi cha Muingereza, Stewart Hall. Farid Musa na Kipre Tchetche wanaweza kupangwa katika safu ya ushambuliaji.
Kipre amekuwa akianzishwa nje katika michezo kadhaa msimu huu. Sijui kwanini, na alitokea benchi na kwenda kuisawazishia timu yake katika mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya vinara hao wa ligi.
Mu-Ivory Coast huyo amekuwa ‘mwiba mkali’ kwa Yanga kwani mara kwa mara amekuwa akiifunga. Tayari amekwishafunga magoli tisa msimu huu, wakati patna wake Bocco amefunga mara 7.
Yanga inataraji kuwa na walinzi wake wote. Nahodha, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Vicent Bossou, Pato Ngonyani, Mbuyu Twite, Juma Abdul, Hajji Mwinyi na Oscar Joshua wote wako fit kwa mchezo huo hivyo itakuwa rahisi kwa mkufunzi, M-holland, Hans Van der Pluijm kufanya machaguo yake katika ngome.
Yanga imeruhusu magoli 9 tu hadi sasa katika ligi, ndiyo timu yenye ukuta mgumu zaidi lakini wanaweza kujikuta wakipoteza mechi mbele ya Azam yenye washambuliaji wengi wenye uzoefu. Bocco, Kipre, Allan Wanga na Mrundi, Didier Kavumbagu pia si wachezaji wa kubeza lakini kiwango chao siku za karibuni kimeonekana kushuka.
Azam imefunga magoli 34 (magoli kumi) pungufu ya Yanga. Amis Tambwe alionekana kushindwa kucheza vizuri na Malimu Busungu katika mchezo wa klabu bingwa wikendi iliyopita, lakini alionekana kucheza vizuri na Paul Nonga katika mchezo huo dhidi ya Circle de Joachim ya Mauritius.
Tambwe alionekana ‘kummiss’ patna wake Donald Mgoma ambaye hakuwepo kutokana na kuhudhuria msiba wa mdogo wake aliyefariki kwao Zimbabwe katikati ya wiki iliyopita. Yanga imefunga magoli 44 (mengi kuliko timu zote) kutokana na ushirikiano mzuri wa Tambwe na Ngoma ambao tayari wamefunga jumla ya magoli 26.
Beki ya Azam FC chini ya Mu-ivory Coast, Paschal Wawa imekuwa ikiwazima Yanga na licha ya kwamba, Hall atawakosa, Aggrey Morris na Erasto Nyoni wachezaji kama David Mwantika na Said Mourad wanaweza kuziba mapengo hayo na kushirikiana vizuri na Wawa, naye Shomari Kapombe ambaye ametajwa kama mchezaji bora wa VPL wa mwezi Januari. Beki ya Azam imeruhusu magoli 11 hadi sasa.
Salum Abubakary, Himid Mao, Mnyarwanda, Jean Mugiraneza, Frank Domayo wanaweza kuanzishwa katika kiungo upande wa Azam wakati Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Mbuyu wakitaraji kuanza katika eneo hilo upande wa Yanga.
Wachezaji wa kati wa Azam wamekuwa wakitumia nguvu na mchezo wa kupasiana ili kupeleka mipira mbele kila wanapokutana na Yanga, hawachoki haraka na hilo limekuwa likichangia sana ugumu wa mechi upande wa Yanga ambao wamekuwa wakipitisha mipira mirefu kutoka nyuma kwenda safu ya mashambulizi.
Mechi hii ni muhimu sana kwa kila timu katika kampeni yao ya kutwaa ubingwa na atakayepoteza atakuwa anatoa nafasi zaidi kwa mwenzake kwenda juu. Nani mshindi wa mechi hii? Hii ni vita ya ubingwa tu.