
Na Abubakar Khatib ‘Kisandu’, Zanzibar
Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Salum Bausi ndoto zake zipo palepale za kuwa Rais wa chama cha soka Zanzibar (ZFA) ambapo baada ya jana kamati ya uchaguzi ya ZFA kutangaza tarehe ya uchaguzi Bausi amesema nia yake ipo palepale na atagombea nafasi ya Urais wa ZFA.
Bausi amesema ana lengo la kubadilisha soka la Zanzibar ambapo yeye atagombea nafasi ya Urais na atatangaza siku ambayo atakayokwenda kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
“Nia yangu ipo pale pale na nimefurahi kuona kuchukua fomu ni shilingi laki mbili tu, kwasababu mwanzo tulisikia laki tano, nia yangu na dhamira yangu ipo palepale na ninaamini nitalikomboa soka la Zanzibar nikiwa kama Rais wa ZFA, mimi ni mtu pekee ninayeweza kuliokoa Jahazi hili ambalo linazama”, alisema Bausi.
“Mimi ndiyo mtu sahihi wa kuongoza soka, kwasababu niliwahi kucheza timu ya taifa, nimewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar tena kwa mafanikio na ndiyomaana nataka kukomboa soka letu la Zanzibar”.
Katika uchaguzi wa mwaka 2012 Kocha Salum Bausi alichukua fomu ya kugombania nafasi hiyo lakini aliishia njiani mwishoni ambapo wadau wengi wa soka bado wanahofu kubwa kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo 3 za juu kwenye chama hicho ambapo wakiamini hata wakigombea hawatoshinda nafasi yoyote kutokana na viongozi waliokuwepo madarakani ni vigumu kuwang’oa.
Jana Kamati ya Uchaguzi ya chama cha soka Zanzibar (ZFA) ilitangaza rasmi tarehe ya kufanyika uchaguzi wa ZFA ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao wa April.
Katika uchaguzi huo nafasi tatu zitakazogombaniwa ambazo ni Urais wa ZFA, Makamu wa Urais ZFA Unguja na Makamu wa Urais ZFA Pemba ambapo fomu za kuwania nafasi hizo zitauzwa kwa shilingi laki mbili.