
Kocha mpya wa Nigeria Sunday Oliseh (katikati) wakti akitambulishwa rasmi kama kocha mkuu wa ‘Super Eagles’
Na Simon Chimbo
Mara baada ya kurithi mikoba ya kocha Stephen Keshi kukinoa kikosi cha Nigeria mwezi julai mwaka huu, kocha Sunday Oliseh (40) ataanza mtihani wake wa kwaza muhimu dhidi ya Taifa Stars Jumamosi hii.
Ingawa Stars iko nyuma ya Nigeria kwa nafasi 87 katika viwango vya FIFA, lakini bila shaka Tanzania itatoa changamoto kubwa dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika ambao wameanza kuunda upya timu yao kupitia Oliseh.
Katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Jumatano hii dhidi ya Abuja Academy, Oliseh alionekana hatulii katika benchi huku mara kwa mara akizungumza na msaidizi wake Francois Vainker.
Wakati wa mapumziko, Oliseh aliwaelekeza wachezaji wake wa mbele namna ya kukaa kwenye nafasi huku akimkazania zaidi Emmanuel Emanike ambaye pamoja na kufunga goli la kwanza rahisi, hakua na mchezo mzuri.
Kuelekea mchezo wa Jumamosi, Oliseh hatakua na mchezaji mzoefu zaidi kikosini golikipa Vicent Enyeama (101 caps) aliyeomba kuondolewa kikosini kwa kile kinachoelezwa kafiwa na mama yake. Carl Ikeme wa Wolverhampton Wanderers anatarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa akiwa na umri wa miaka 29.
Mbele ya golikipa, wapo walinzi William Troost-Ekong ambaye atacheza mechi yake ya pili katika timu ya taifa pamoja na Kenneth Omeruo huku walinzi wa pembeni wakitarajiwa kuwa ni Kingsley Madu na Solomon Kwambe.
Sehemu ambayo Nigeria inaweza kuhangaika ni sehemu ya kiungo kutokana na Nwankwo kutokuonesha kitu katika sehemu ya kiungo cha ulinzi pamoja na kwamba Simon Moses kuonesha uwezo mzuri katika winga ya kushoto huku Musa akiwa pia tishio upande wa kulia.
Akiulizwa kuhusu timu yake kutokuwa na mchezaji mwenye kipaji kama Messi, Sunday Oliseh anasema anaamini katika timu na sio mchezaji mmoja mmoja kutokana na ukweli kwamba italeta shida siku anayetegemewa akikosekana.
Akija na wachezaji sita kutoka ligi ya nyumbani ya Nigeria, Oliseh ana matumaini makubwa kuwa kutokana na alichokiona mazoezini, basi pia yanaenda kuoneshwa uwanjani katika mechi.
Nigeria kama taifa ‘kichaa’ la soka halina tarajio lolote zaidi ya ushindi Dar es Salaam, lakini Oliseh anapunguza matarajio ya wengi na kusema kuwa bado yuko katika kujenga timu kwamba hatoangalia zaidi ushindi bali namna gani wanacheza.
Oliseh atakua akiangalia pia mchezo wa kundi ‘G’ kati ya Egypt na Chad. Mafarao wanaongoza kundi kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.