
Kocha mkuu wa timu ya Mbeya City Kinnah Phiri ametaja sababu iliyopelekea kikosi chake kupoteza mchezo wao dhidi ya Yanga kwenye uwanja wao wa nyumbani (Sokoine) kwa kipigo cha magoli 2-0.
Mmalawi huyo amesema uzoefu wa wachezaji wa Yanga ndio sababu kubwa iliyowapa ushindi kwenye mchezo wa leo huku akisema kukosa uzoefu kwa washambuliaji wake kumewafanya washindwe kupata bao kwenye mechi ya leo.
Phiri ambaye amejiunga na City kuchukua mikoba ya mzalendo Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema, timu yake imecheza vizuri lakini kitu kilichowafanya wapoteze mchezo wao ni uzoefu wa wachezaji wa Yanga na si vinginevyo
“Tulikosa umakini kwenye safu yetu ya ushambuliaji lakini tumecheza vizuri nja kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ambazo tumeshindwa kutendea haki”, anasema Phiri aliyechukua mikoba ya kocha mzalendo Meja Mstaafu Abdul Mingange ambaye aliachwa na mabosi wake wa Halmashauri ya jiji la Mbeya.
“Kama ulivyoona, tumetengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tulishindwa kufunga. Wapinzani wetu wametufunga kutokana na uzoefu wao hakuna kingine”.
City waliruhusu goli la kwanza dakika ya 16 likifungwa na beki wa Yanga mtogo Vicent Bosou ambaye liruka bila kukabwa na kuukwamisha mpira wavuni.
Uzoefu wa mlinda mlango wa Mbeya City Juma Kaseja uliwasaidia Mbeya City kutokana na kufanya kazi ya ziada kuokoa michomo ya washambuliaji wa Yanga ambao waliliandama goli la City kila mara.
Mrundi Amis Tambwe akaifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju mkali ambao aliuachia akiwa nje ya box huku Kaseja akiwa hakutarajia kama Tambwe angenyoosha bakora kwa umbali aliokuwepo.