
Baada ya Yanga SC kufanikiwa kutetea ubingwa wao wa ligi kuu ya kandanda Tanzania Bara (VPL) ushindani na vita kali zaidi sasa umebaki miongoni mwa timu tano ambazo mbili zitapaswa kuteremka daraja hadi ligi daraja la kwanza kuungana na Coastal Union ya Tanga ambayo tayari imeshuka.
Toto AFRICANS
Toto Africans ya Mwanza itakuwa wageni wa Tanzania Prisons ya Mbeya katika uwanja wa Sokoine mwishoni mwa wiki hii wanalazimika kupambana katika michezo yao miwili iliyosalia ili kuepuka kushuka kwa maana licha ya kuwa nafasi ya 11 katika msimamo wanaweza kuteremka kama watashindwa kupata walau alama moja katika game zao dhidi ya Prisons kisha Stand United katika uwanja wa CCM Kirumba siku ya mwisho ya msimu. Pointi 30 walizonazo zinaweza kufikiwa na Mgambo JKT, Kagera Sugar, African Sports na JKT Ruvu.
JKT RUVU
Ikiwa ametangaza kuhitaji kupumzika kazi ya ufundishaji, mkufunzi Abdallah ‘King’ Kibadeni anapambana kuhakikisha JKT Ruvu haishuki daraja kwa mara ya kwanza ikiwa mikononi mwake. Game dhidi ya JKT Mgambo ni zaidi ya fainali ya kikombe kwani mshindi atakuwa ni kama amejihakikishia kubaki VPL.
Ruvu wataenda Tanga, Jumamosi hii wakitambua kuwa pointi zao 29 hazitoshi kuwabakisha ligi kuu hivyo pointi moja dhidi ya Mgambo itakuwa na maana kubwa sana kwao siku ya Jumamosi kwa maana watacheza tena na Simba SC, Mei 21 mchezo wao wa mwisho.
Wapo nafasi ya 12, nyuma ya Toto iliyo nafasi ya 11, pointi 3 zaidi ya Sports iliyo nafasi ya 13, pointi nne zaidi ya Kagera Sugar na pointi 5 zaidi ya Mgambo.
AFRICAN SPORTS
Timu pekee ya Tanga ambayo labda inaweza kusalia VPL msimu ujao. Sports imekuwa chini ya msimamo kwa muda mrefu na huku zikiwa zimebaki game mbili mikononi mwao dhidi ya Azam FC wikendi hii katika uwanja wa Mkwakwani, Sports hawatashuka ikiwa watashinda game zao mbili za mwisho. Wana alama 26 katika nafasi ya 13.
KAGERA SUGAR
Umekuwa msimu mbaya sana kwa Kagera na ili wasalie VPL watalazimika kuifunga Stand United wikendi hii kisha kuwafunga Mwadui FC siku ya mwisho ya msimu na kusubiri hatma yao kwa kusikilizia matokeo ya timu nyingie. Kagera itakuwa mwenyeji wa game zote mbili za mwisho.
MGAMBO JKT
Itacheza na JKT Ruvu Mei 14 na ikiwa watapa ushindi watafikisha alama 27. Sare dhidi ya Azam FC katika uwanja wa Chamanzi katika game ya mwisho msimu uliopita iliwabakisha VPL.
Kuishinda JKT Ruvu katika uwanja wa Mkwakwani itawafanya waende tena Azam Complex siku ya mwisho kujaribu kufanya kile walichofanya msimu uliopita. Bingwa wa VPL tayari amepatikana lakini sasa utamu wa VPL ni huku chini ya msimamo ambako kunahitajika kuona timu nyingine mbili zikiteremka daraja kuifuata Coastal Union.