Ikiwa zimesalia saa kadhaa ili pambano la watani wa jadi kadi ya Simba na Yanga lipigwe kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kupitia kwa afisa habari wake Baraka Kizuguto limetoa tahadhari kuwa, mashabiki wa soka wataokwenda kushuhudia mchezo huo wasivae mavazi yatakayoashiria hisia zao, upande au ushabiki wa vyama vya siasa wanavyovishabikia.
Kizuguto ameongeza kuwa, vitu vingine kama vinywaji, silaha, mabegi na vitu vyovyote vyenye kuhatarisha amani na usalama uwanjani havitaruhusiwa kuingia uwanjani.
Hatua hiyo imekuja baada ya kutokea kwa matukio ya ushabiki wa vyama vya siasa kwenye mchezo kati ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stsrs’ dhidi ya Nigeria mapema mwezi huu ambapo mashabiki wa soka walishindwa kuzuia hisia zao juu ya vyama wanavyovishabikia huku wengine wakionekana kupeperusha bendera za vyama vyao.
Katika hatua nyingine Kizuguto amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika kwa upane wa TFF huku akisema pia jeshi la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha mchezo huo unachezwa katika hali ya amani na utulivu bila kusababisha uvunjifu wa amani.