Leo nimepata fursa ya kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari na kocha wa Atletico ambaye aliongozana na wachezaji wake Gabi pamoja na Fernando Torres kwaajili ya kuzungumzia mchezo wa fainali ya Champions League itakayofanyika kesho kwenye uwanja wa San Siro hapa mjini Milan, Italy.
Katika mazungumzo ya Simeone kuelekea mchezo wa kesho, amempongeza kocha wa Real Madrid kwa kufanikiwa kusuka upya timu yake na kuifanya kuwa mpya na bora kwa muda mfupi tangu alipoichukua.
“Zidane amefanya kazi kubwa kukisuka kikosi cha Real Madrid kwa kipindi cha muda mfupi alichokaa na kikosi hicho, amefanya uamuzi mkubwa wa kumuamini na kumpa nafasi kiungo Casemiro, ameifanya timu nzima kuwa imara. Casemiro ndiye mchezaji muhimu kwasasa kwenye kikosi cha Real Madrid”, hayo ni maneno ya Diego Simeone wakati anazungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa fainali ya klabu bingwa Ulaya.
Mshambuliaji wa Atletico Madrid Fernando Torres amesema, kuchukua taji la mabingwa Ulaya akiwa na Atletico itakuwa ni jambo jema licha ya kuwahi kutwaa taji hilo wakati akiwa na klabu ya Chelsea ya England.
“Licha ya kushinda mataji kadhaa nikiwa na timu ya taifa ya Hispania pamoja na kutwaa taji la taji la UEFA nikiwa na Chelsea mwaka 2012, nikishinda taji hili nikiwa na na Atletico litakuwa muhimu sana kwenye maisha yangu”, amesema Fernando Torres ambaye aliifungia Atletico bao pekee kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali wakati Barca inaifunga Atletico kwa magoli 2-1 kwenye uwanja wa Camp Nou.