Nahodha wa timu ya Yanga Nadir Horoub ‘Cannavaro’ amesema licha ya timu yake kuibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya mahasimu wao Simba, anawapongeza Simba kwa kucheza vizuri hasa katika kipindi cha kwanza cha mchezo wao.
Cannavaro alikiri kuwa, Simba walicheza vizuri lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata na akaongeza kwamba si vibaya kusema ukweli kwani kila mtu aliona Yanga ilipotea eneo la katikati na kuwafanya Simba kucheza wanavyotaka na kusababisha washambulie kwa muda mwingi wa kipindi cha kwanza.
“Nawapongeza sana Simba wamecheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini ukiweza kuwazuia Simba wasikufunge ndani ya dakika ishirini za kwanza basi unashinda game”, alisema Cannavaro.
“Sisi tumejipanga vizuri kwa kila mechi ambayo ipo mbele yetu lazima tunshinde. Wanayanga wafurahie ushindi huu na waendelee kutuamini, sisi tunawaahidi kila tutakapokutana na Simba kichapo kitaendelea”.
“Kwa upande wetu tumezitumia vizuri nafasi tulizozipata na kuweza kuibuka na ushindi, wenzetu walitengeneza nafasi pia lakini hawakuweza kufunga. Kwenye mpira ni muhimu sana kucheza na nafasi maana unapopoteza nafasi huwezi jua kama mnaweza kutengeneza nafasi nyingine, inaweza ikawa ndiyo hiyo pekee mliyoipoteza”.