Na Naseem Kajuna
Michuano ya Euro 2016 imeendelea jana kwa droo ya 0-0 kwenye mechi ya Ufaransa dhidi ya Switzerland na ushindi wa 1-0 wa Albania dhidi ya Romania
Na leo kutakuwa na mechi nyingine kati ya England na Slovakia na timu ya Russia itakayocheza na Wales.
Lakini je ulishawahi kujiuliza kwanini mechi za mwisho za hatua ya makundi huchezwa pamoja wakati zingine zote huchezwa wakati tofauti sababu ni hii hapa.
Algeria walifanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki kwenye kombe la dunia la 1982 nchini Spain, kombe la dunia la mwaka huo lilikuwa lishafunguliwa kwa matokeo ya ajabu pale timu ya Belgium ilipowafunga mabingwa wa dunia watetezi Argentina 1-0, lakini wachache sana walitambua kwamba maajabu ndiyo kwanza yalikuwa yanaanza.
Wengi waliamini kwamba mechi ya kwanza ya kundi la pili kati ya West Germany na Algeria ingeisha kwa ushindi wa kishindo wa West Germany ambao kwa wakati huo ndiyo walikuwa mabingwa wa Bara la Ulaya. Wajerumani waliweza kufuzu kushiriki mashindanio hayo kwa kishindo baada ya kushinda mechi zao zote nane za kufuzu wakifunga magoli 33 na wao wakifungwa goli 3 pekee.
Timu yao ilikuwa imejaa nyota lukuki wa wakati huo kama vile Karl Heinz Rummenige, Paul Breitner na wengineo. Wajerumani walikuwa na uhakika na ushindi kwenye mechi na Algeria kiasi kwamba walijifurahisha kwenye mkutano kabla ya mechi hio kwa kuwatania wa Algeria “Goli letu la saba litakuwa kwa ajili ya wake zetu na la nane kwa ajili ya mbwa wetu,” alisikika akisema mchezaji mmoja wa West Germany.
Kocha wao Jupp Derwall hata aliapia kwamba endapo timu yake ingefungwa mechi hiyo basi angerukia mbele treni ya kwanza inayorudi mjini Munich.
“Mchezaji mmoja ata alisema kwamba atacheza na sisi huku anavuta sigara mdomoni” anakumbuka beki wa kushoto wa timu ya Algeria ya enzi hizo Chaabane Merzekane ambaye alikuja kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
“Wengi wetu tulizani kwamba walikuwa wanasema vitu hivi ili kutudanganya tu, kutufanya tufikirie kwamba hawakuchukulia timu yetu Serious na kwamba hawakutufanyia utafiti, lakini ulishawahi kusikia wapi timu ya kijerumani ambayo haijaifanyia utafiti timu Pinzani.”
Cha ajabu ni kwamba timu hii ya Ujerumani haikuifanyia timu ya Algeria utafiti kweli. Kocha wao Derwall baada ya mechi alikubali kwamba alipewa video ya timu ya Algeria lakini hakuwaambia wachezaji wake waitazame kwa hofu kwamba wangemcheka.
Endapo Wajerumani wangetumia muda wao kutazama video hile basi wasingetumia muda wao kuwatania wa Algeria kwani wangekuja kutambua kwamba mpinzani wao wa mechi hiyo alifuzu kwenye mashindano hayo baada ya kumfunga Nigeria nyumbani na ugenini na alijiandaa kwa mashindano hayo kwa mechi zilizozalisha ushindi dhidi ya Republic of Ireland, Benfica na hata Real Madrid.
Wajerumani pia wangegundua kwamba wa Algeria wanacheza mpira wa kasi na kwamba wachezaji wa Algeria wanauelewano mkubwa sana uwanjani kwa sababu wachezaji wote hawa walikuwa wakicheza pamoja kwa miaka mingi sana, na wengi wao walikuwa wanacheza nyumbani kwao kwa sababu sheria za Algeria kwa wakati huo zilikuwa zinakataza wachezaji kuhama nchini Algeria kabla ya kufikisha miaka 28.
Wajerumani walishanganzwa kwenye mechi hiyo, Algeria waliwashambulia wajerumani mwanzo mwisho huku Merzekane akimtesa sana Breitner ,“Nilisikia kwamba Breitner anapenda kushambulia sana, kwamba yeye ndiyo alikuwa bora zaidi duniani kwa hilo mimi nikaona huo ndiyo udhaifu wake kwa hiyo nikautumia,” alisema Merzekane.
Algeria walitamba kipindi cha kwanza na walifanikiwa kupata goli dakika ya 54, Rumenigge alirudisha goli hilo dakika ya 67 lakini kama wajerumani walidhani kwamba mambo yatakuwa sawa tena walikosea.
Wa Algeria waliweza kutengeneza goli baada ya kupiga pasi 9 golini na mchezaji Belloumi kumaliza vizuri karibia na goli. Lilikuwa kati ya magoli bora kwenye michuano hiyo. Kiukweli Algeria walikuwa na uwezo wa kushinda mechi ile hata kwa goli tatu au nne.
Wa Algeria waliwapa Ujerumani heshima yao baada ya mechi hiyo na hawakushangilia kwa fujo
Algeria walifungwa kwenye mechi yao ya pili dhidi ya Austria bila shaka ikichangiwa na timu ya Austria kuogopa sana uwezo Algeria iliouonesha kwenye mechi yao dhidi ya Ujerumani na kujipanga ipasavyo, ila waliweza kupata magoli matatu ya haraka dhidi ya Chile kwenye mechi ya tatu ya kundi. Lakini Algeria walionesha ukosefu wao wa uzoefu kwenye michuano mikubwa kwa kuruhusu Chile kurudisha magoli mawili.
Algeria alishinda mechi hiyo 3-2 na matokeo haya yalihakikisha kwamba ingekuwa timu ya kwanza kutokea Barani Afrika kufuzu kwenda kwenye hatua nyingine ya michuano. Matokeo pekee ambayo yangeitoa Algeria ni ushindi wa goli moja au mawili kwa timu ya Ujerumani dhidi ya Austria siku inayofuata, matokeo ambayo yangepeleka wote Austria na Ujerumani kwenye hatua inayofuata.
Katika dakika ya 10 ya mechi hiyo Ujerumani alitangulia mbele na hakikutokea kingine chochote mpaka mwisho wa mechi hiyo timu zote mbili ziliacha kucheza kwani matokeo hayo yalikuwa yanawafaa wote wawili. Katika dakika 80 zilizofuata halikupigwa shuti lolote na wala hamna hata mchezaji aliyejisumbua kukimbia, wachezaji wa timu zote mbili walikuwa wakipiga pasi hapa na pale golini kwao na pale walipofika golini walifanya vitendo vya jabu kwa maksudi kama vile kuteleza ama kupiga mpira nje kabisa. Hii haikuwa mechi tena huu ulikuwa mpango.
Mashabiki wa Algeria uwanjani humo walichoma fedha kuashiria kuhisi kwamba wametapeliwa kwenye mechi hiyo. Kitendo hiki kiliudhi hata wananchi wa Austria na Ujerumani pia .Mtangazaji mmoja wa Kijerumani alisikika akitamani hata kulia wakati mechi hii inaendelea na wakati mtangazaji wa Austria yeye aliwaambia watazamaji wake wazime luninga zao na hakuongea tena kwa nusu saa ya mwisho ya mechi hiyo.
Ila mkuu wa kikosi cha Austria yeye hakuonesha hata kusumbuliwa na kitendo hiki, yeye aliongea maneno haya “Mchezo wa leo umechezwa kwa mbinu lakini kama hawa watoto 10,000 kutoka jangwani wanataka kuleta gumzo kuhusu hili basi inaonesha kwamba hawana shule za kutosha. Yani sheikh anatoka jangwani huko na anaruhusiwa kunusa hewa ya kombe la Dunia kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 300 halafu anadiriki kufungua domo lake.”
Tukio hili linakumbukwa milele kama aibu ya Gijon na kwa sababu ya tukio hili na mengineo yafananayo na hili FIFA iliamua kwamba mechi zote za mwisho za hatua ya makundi kwenye michuano yeyote ile itachezwa kwa pamoja.
Kwa upande wao wa Algeria wao hawakuwa na nongwa. Baada ya mechi mshambuliaji wao Belloumi alisema “Kuona wababe hawa wa dunia wawili wakijiaibisha ili tu kumtoa Algeria ni heshima kwetu. Sisi tumetoka na vichwa vyetu juu wakati wao wametoka na aibu…..Uwezo wetu ulifanya FIFA wafanye mabadiliko hayo na hicho ni kitu kizuri zaidi hata haya ushindi.”