Na Baraka Mbolembole
Mechi 9 mfululizo bila ushindi! Nadhani sasa imetosha, na mabingwa mara 26 wa Tanzania Bara, timu ya Yanga SC wanapaswa sasa ‘kuwalipa’ mashabiki wao kwa kupata ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi michuano ya CAF.
Ndiyo, Yanga wamekuwa ‘wa-kwanza’ katika matukio mengi ya kihistoria katika ngazi ya kimataifa lakini mahasimu na wapinzani wao wa jadi katika soka la Tanzania, Simba SC wamekuwa na matokeo bora zaidi yao kimataifa kila wapofanikiwa ‘kuvuka vikwazo.’
Ndani ya soka la Tanzania, Yanga ni timu yenye vikombe vingi zaidi kuliko timu nyingine yoyote ile lakini matokeo ya ‘wenyewe kwa wenyewe’ dhidi ya Simba bado wanaendelea kupelekeshwa na vipigo vya 6-0, 5-0, 4-1, 4-1, huku upande wao ni mara moja tu wameweza kuishinda 5-0 timu ya Simba.
Mataji 6 zaidi ya ligi dhidi ya Simba yanawafanya Yanga waendelee kubaki klabu bora zaidi ya muda wote nchini. Lakini inapotokea mshabiki wa Simba na kuiweka Yanga katika mizani na timu yake, atashinda tu. Huu ndio ukweli.
Timu ya kwanza ya Tanzania kucheza nane bora ya michuano ya Caf ni Yanga. 1969 na 1970 historia inatuambia kwamba ‘timu ya wananchi’ ilifika robo fainali mbili mfulululizo katika iliyokuwa ‘klabu bingwa Afrika,’ sasa ligi ya mabingwa.
Lakini ni Simba pekee ambayo historia inatuambia iliwahi kufika nusu fainali katika michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu barani Afrika. 1974 Simba ilitolewa na Mehala El Kubra ya Misri.
Pamoja na kwamba Yanga walikuwa ndiyo timu yenye mataji mengi ya ligi- Bara, Simba inabaki kuwa timu yenye matokeo bora zaidi katika ngazi ya kimataifa. Ilifika fainali za kombe la Caf (sasa Caf Confederation Cup) mwaka 1993. Pia ndiyo klabu bingwa mara nyingi zaidi ukanda wa Cecafa (mabingwa mara 6, mara moja zaidi ya Yanga.)
Yanga ni miongoni mwa timu 8 za kwanza Afrika ambazo ziliunda makundi mawili ‘A na B’ wakati Shirikisho la soka Afrika-Caf lilipobadili mfumo wa michuano ya klabu-kutoka timu kucheza home na away katika mtindo wa mtoano-mwazo hadi mwisho wa michuano na kuwa ‘Ligi ya mabingwa 8.’
Lakini michezo yote 6 waliyofanikiwa kucheza mwaka 1998, mabingwa hao wa Tanzania Bara hawakupata ushindi wowote ule zaidi ya sare katika game zao mbili kati ya 3 za nyumbani.
Lakini Simba ilipofanikiwa kufika hatua hiyo mwaka 2003 waliweza kushinda game mbili dhidi ya Asec Mimosas na walioenda kushinda taji, timu ya Enyimba huku wakitoa sare moja nyumbani dhidi ya Ismailia na nyingine ugenini dhidi ya Asec.
Simba walipoteza game mbili za ugenini dhidi ya Enyimba na Ismailia. Walimaliza michezo 6 wakiwa na alama 8, pointi 7 wakipata uwanja wa nyumbani.
Ukirudisha kumbukumbu-kihistoria utagundua kuwa Yanga ‘wana-safa sana’ katika ngazi ya kimataifa licha ya kwamba wamecheza mara 21 michuano ya mabingwa Afrika. Uzoefu tayari wanao wa kutosha na ndiyo uliowasaidia kuwafunga na kuwaondoa katika michuano timu changa kimataifa ya Esperanca kutoka Angola na kufuzu kwa mara ya kwanza katika makundi ya Caf Confederation Cup 2016.
Michezo yao miwili ya nyumbani imekuwa na matokeo ‘hasi’ na ule mmoja wa ugenini dhidi ya MO Bejaia ulikuwa na matokeo mabaya. Kufungwa na TP Mazembe katika uwanja wa Taifa ilikuwa ni ‘sawa kwa walio wengi’ ambao waliamini kipigo cha 1-0 kilistahili kwa mabingwa wa Bara.
Sare yangekuwa ni matokeo mazuri lakini tuliitazama Mazembe kama mabingwa wa ligi ya mabingwa 2015 kuliko uwezo wa sasa wa timu ya Yanga.
Yanga haikupaswa kufungwa na Mazembe hapa, lakini kiwango kabambe kilitoa matumaini ya kuwashinda Waghana, Medeama SC katika mchezo wa 3 lakini mambo yakaenda ‘mrama’ na pengine ilikuwa siku ambayo mashabiki walishuhudia kiwango cha chini cha umaliziaji kutoka kwa safu yao ya mashambulizi.
Nafasi ya wazi aliyopoteza mshambulizi, Amis Tambwe dakika chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili usingeamini kuwa mfungaji huyo bora zaidi VPL kwa miaka mitatu sasa ndiye alikosa goli akitazamana na golikipa tu.
Nafasi ya wazi aliyopeza Obren Chirwa kipindi cha kwanza unaweza kupingana na mtu anayekuambia huyo ndiye mchezaji ghali zaidi katika mpira wa Tanzania-anathamani ya zaidi ya milioni 200 tena ametoka ng’ambo ya nchi.
Nilimuhurumia sana mkufunzi, Hans Van der Pluijm mara baada ya Medeama kusawazisha goli la Donald Ngoma dakika 16′ tu baada ya wao kufunga. Hans alikuwa akipiga kelele mara kwa mara kuwakumbusha wachezaji wake wa nafasi ya ulinzi kuhusu umakini, lakini alionekana kuchukizwa mno na namna safu yake ya mashambulizi ilivyokuwa ikipoteza nafasi.
Yanga wanazuia vizuri na kuruhusu goli 3 katika game 3 si mbaya ila yanaumiza inapotekea mmefungwa Mazembe kisha Medeama wanapata sare nyumbani huku wote wakifunga kwa stahili ya kufanana-mipira iliyokufa.
Mashabiki wengi wa Yanga wameonekana kukata tamaa ya timu yao kusonga mbele huku pia wakisema wanajiandaa na michuano ya mwaka ujao! Utakaje tama wakati kuna pointi 9 mbele yako?
Si hivyo tu, hata kabla ya kuanza kwa michuano ya Caf, Februari mwaka huu hakuna ‘mwana michezo’ ambaye alikuwa akiipa Yanga nafasi ya kuwa miongoni mwa timu 8 bora, lakini baada ya kufuzu kwa hatua hiyo wengi tunaamini kuwa Yanga wanaweza kusonga mbele zaidi ya hapo.
Niliamini Yanga wangepata ushindi wa kwanza dhidi ya timu za kiarabu walipokwenda kucheza na Waalgeria, MO Bejaia katika game yao ya kwanza, lakini haikuwa hivyo. Wakachapwa 1-0, bado sikuvunjika moyo, nikaamini Yanga wataifunga TP Mazembe katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini wapi. Wakachapwa 1-0.
Lakini nikajifunza kitu kutoka kwa shabiki Mcongoman ambaye alitoka Lubumbashi kuja kuisapoti Mazembe hapa nchini. Alisema Yanga ni ‘wamataifa’ na Mazembe wamekuja kudhirisha hilo kuwa timu ya kimataifa ni wao.
Daah! Nilimuelewa sana, kwamba Yanga watabaki washindani wa baadhi ya mataifa tu, na kimataifa ni ‘levo’ za TP Mazembe. Ila naye alikuja Dar akijua kuwa Yanga wanajiita wa kimataifa ndiyo maana baada ya dakika 90′ akasema alichopata kukisikia.
Niliamini Yanga wangepata ushindi wao wa kwanza makundi Caf dhidi ya Medeama lakini nilikuwa nikiomba mpira uishe! Ngoma ikaisha 1-1.
Mechi yao ya kumi kihistoria makundi Caf, huu sasa ni wakati wa malipo Yanga SC kwa mashabiki wao. Watalazimika kuboresha umakini tu katika kujilinda na umaliziaji ili kuishinda Medeama kwao.
Timu hiyo changa kimataifa kutoka Ghana iliwashambulia mno Yanga katika uwanja wa Taifa lakini naamini kibao kitawageukia Waghana hao katika game ya Jumanne hii wakiwa nyumbani kwao.
Walishangiliwa sana walipokuja Dar es Salaam. Sidhani kama itakuwa hivyo na kwao Ghana na Yanga wamekuwa wakicheza vizuri zaidi kuliko nyumbani katika game zao za kimataifa.