Mchezaji mkongwe wa Simba SC Musa Hassan Mgosi kesho (Jumapili August 14) ataagwa rasmi kama mchezaji wa klabu hiyo atakapokuwa akistaafu rasmi kucheza soka la ushindani.
Mgosi ataagwa kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Simba dhidi ya URA ya Uganda utakaochezwa kwenye uwanja wa taifa.
Kuelekea mchezo huo, afisa habari wa Simba SC Haji Manara amethibisha kwamba Mgosi atalipa soka kisogo na amepewa nafasi ya kuwa meneja wa klabu hiyo mara baada ya kutangaza kustaafu.
“Licha ya kwamba mechi dhidi ya URA itawapa fursa benchi la ufundi kuangalia na kufanya masahihisho ya mwisho kabla ya ligi kuu kuanza wiki ijayo, tutatumia mechi hiyo pia kumuaga mchezaji wetu Musa Hassan Mgosi ambaye tayari anastaafu rasmi kucheza soka la ushindani,” amesema Manara.
Haji amesema Mgosi atacheza ,mechi hiyo kwa dakika chache kisha baadaye atastaafu kwa kushika mpira na kuubusu na kufanya mambo mengine ambayo hufanywa wakati mchezaji anapotangaza kustaafu kisha kuwapungia mkono mashabiki.
Msemaji huyo wa Wekundu wa Msimbazi aliendelea kusema kwamba, baada ya zoezi la kustaafu, Mgosi ataingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ambapo atabadili nguo na kurudi uwanjani akiwa kama maneja .
“Baada ya Mgosi kustaafu anakuwa meneja mpya wa Simba wakati Abasi Ali ataendelea kuwa mratibu, kwa pamoja watu hawa wawili watakuwa wanashirikiana huku mmoja akiwa karibu zaidi na benchi la ushindi kwa maana ya Mgosi na mwengine akifanya logistics za kawaida za timu nje ya benchi la ufundi lakini kwa ushirikiano wa ndani.”
“Tunafanya hivi kwa ajili ya kuwapa motisha wachezaji vijana kwamba unapocheza klabu ya Simba kwa juhudi, nidhamu na mafanikio unaendelea kuwa sehemu ya Simba. Kwahiyo tunampa nafasi hiyo mgozi tunajua ni mchezaji aliyejituma sana, mwenyenidhamu kubwa na uzoefu wa kutosha atashirikiana na uongozi kuhakikisha msimu huu tunafanya vizuri.”