Na Faraji Fowz Zeggeson
Tasnia ya muziki imekuwa bega kwa bega na michezo hata imekuwa ikiingiliana wapenzi .Yani wanaopenda michezo na muziki kwa wakati mmoja.
Tumeona mara nyingi tu wanamuziki wakitunga mashairi yao wakijifananisha uwezo wao wa kimuziki na baadhi ya wanamichezo na hawajaishia tu katika mashairi yao bali hata wengi wao hutunga nyimbo zao na kuita nyimbo zao majina ya wanamichezo mfano Mwana Hiphop wa nchini Marekani The Game mwaka 2012 kutoka katika albam yake ya tano aliachia wimbo unaokwenda kwa jina la ‘ALI BOMAYE ‘.
ALI BOMAYE katika lugha ya kilingala ina maana ya ‘ALI MUUE’ kwa Kiswahili na hii ilitokea katika pambano la kihistoria lililowahi kutokea duniani katika mchezo wa masumbwi baina ya MUHAMMAD ALI na GEORGE FOREMAN katik ardhi ya Congo mnamo mwaka 1974 ambapo mashabiki waliokuwa wakiutazama mchezo huo walikuwa wakimpigia mayowe na kumuamuru MUHAMMAD ALI amuue GEORGE FOREMAN ‘ALI BOMAYE’ (Ali Kill Him).
Hata mwanamuziki kutoka Tanzania, Ali Kiba alitumia kionjo hicho katika wimbo wake wa ‘Unconditionally Bae’ alioshirikiana na Sauti Sol Kutoka Kenya. Rapper kutoka Kenya Khaligraph Jones Septemba 2 mwaka 2015 alitoa wimbo unaitwa ‘JULIUS YEGO’ Akifananisha uwezo wake mkubwa wa ku-rap kama mwanariadha huyo wa nchini Kenya mwenye mafanikio makubwa na akiwa ndio mwanariadha wa kwanza nchini Kenya kuweza kushinda medali ya dhahabu katika michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2014.
Uhusiano mzuri uliopo kati ya wasanii wa muziki na wana michezo ndio umepelekea hata baadhi ya Wanamichezo kuweza kutumia aina za kucheza za wasanii hao kama aina ya ushangiliaji pindi wanafunga Mabao. Hapa chini nitakuelezea aina ya ushangiliaji ya wanamichezo inayotokana na aina ya kucheza kutoka kwa wasanii wa muziki.
- DAB
Dab ni aina ya kucheza ambapo mchezaji anashusha kichwa chini na kukilaza kwenye kiwiko huku mikono yake yote miwili akiwa ameinyoosha kuelekea juu katika uelekeo mmoja. Aina hii ya uchezaji ina asili kutoka mji wa Atlanta nchini Marekani ambapo wana Hiphop wengi mjini humo walikuwa wakiitumia na ilipata kuwa maarafu sana baada ya kikundi cha wasanii wa Hiphop nchini Marekani ‘MIGOS’ kuachia wimbo wao wa ‘Look at my Dab’ na kupelekea baadhi ya wanamichezo kuitumia kama aina ya ushangiliaji.
CAM NEWTON
Mchezaji wa mpira wa kimarekani katika timu ya CAROLINA PANTHERS ambaye alikuwa kivutio kikubwa katika ligi kuu ya mpira wa kimarekani (NFL). Mchezaji huyu wa nafasi ya robo ya kwanza ya nyuma alionekana kwa mara ya kwanza akisherekea kwa aina ya Dab katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tennessee Titans mwaka 2015. Cam Newton alisema hata tumia tena aina ya ushangiliaji pindi mwaka 2016 utapoingia alipohijiwa na radio ya Charlotte.
JEREMY HILL
Jeremy Hill ambaye naye ni mmoja wa wanamichezo wa awali wa mpira wa kimarekani alionekana akitumia aina hiyo ya ushangiliaji alipofunga katika mchezo wa week ya kwanza baina ya Oakland Raiders Septemba 13 mwaka 2015.
LEBRON JAMES
Mfalme huyu katika Ligi kuu ya Kikapu ya nchini Marekani alionekana kwa mara ya kwanza akicheza aina hii ya Dab baada ya kufunga katika mchezo wa awali kabla ya ligi kuanza (Pre Season) Octoba 5 2015.
FRANK BEAMER
Sio tu wachezaji wameonekana wakivutiwa na aina hii ya uchezaji bali hata Wakufunzi, Frank Beamer ni mkufunzi wa mpira alionekana akishangilia kwa Dab. Kocha huyu wa zamani wa timu ya Virginia Tech baada ya kustaafu kukinoa kikosi hicho, Frank Beamer akabaki kuwa Mkufunzi klabuni hapo. Licha ya kuwa na miaka 70 lakini akaona hawezi kupitwa na ushangiliaji huu wa Dab.
PAUL LABILE POGBA
Kiungo huyu wa Manchester United inawezekana ndio mwanamichezo ambaye anapenda aina hii ya ushangiliaji ya Dab licha ya kuonekana mara kwa mara akishangilia kwa kucheza kwa aina ya Dab vilevile pia alienda mbali zaidi hadi kuamua kujichora neno ‘DAB’ katika upande wa kushoto katika kichwa chake ikiwa kama aina ya unyoaji wake.
Pogba aliitumia sana aina hii ya ushangiliaji alipokuwa na timu yake ya zamani ya Juventus huku alikuwa akipewa kampani na mchezaji mwenzake Paul Dyabala, vilevile huwa anacheza aina hii ya Dab hadi akiwa katika timu yake ya Taifa ya Ufaransa. Na ameonekana pia kuishawishi Brandi ya utengenezaji wa magemu ya video EA SPORTS kwani wameweka wazi kuwa aina hii ya ushangiliaji itapatikana katika gemu ya FIFA 17 pale ambapo Paul Pogba akifunga ataonekana akishangilia kwa uchezaji wa DAB.
JESSE LINGARD
Winga huyu wa Manchester United mwenye asili ya Uingereza ni moja ya wanamichezo wanayoipenda aina hii ya uchezaji, ameonekana mara kwa mara akicheza mchezo huu pindi akifunga. Jesse Lingard amepata patna wakucheza nae katika club ya Manchester United baada ya Kusajiliwa kwa Paul Pogba ambaye pia ni mpenzi wa uchezaji huo.
Jesse Lingard, 23, ameonekana kuwa na furaha baada ya kupata patna wa kucheza nae hasa baada ya Pogba kusajiliwa na Manchester United alipost katika mtandao wake wa instagram picha iliyounganishwa ya kwake na Pogba wakiwa wote wana DAB na wenye ujumbe wa kumkaribisha tena nyumbani. Jesse Lingard alishawahi kukiri kuwa amevutiwa na aina hii ya hchezaji baada ya kumuona Paul Pogba akishangilia kwa Dab pindi alipokuwa katika ligi ya nchini Italia SERIE A.
- HOTLINE BLING DANCE
Aina hii ya Uchezaji inapatikana katika video ya wimbo wa Rapper mwenye asili ya Canada Drake ‘Hotline Bling’ uliotoka mwaka 2015 ambao ni wimbo wa kwanza kuachiwa kutoka katika albamu yake ya nne ‘Views from the Six’.
ANTOINE GRIEZMANN
Mshambuliaji huyu wa kifaransa alikuwa kivutio kikubwa katika michuano ya kimataifa ya Ulaya ya mwaka 2016 kwa aina yake hii ya uchezaji akiwa kama anapiga simu ‘HOTLINE BLING DANCE’.
Mshambuliaji huyu aliyetumbukia nyavuni mara sita katika michuano hiyo alisema pia alikuwa akiitumia aina hii ya ushangiliaji hata pindi alipokuwepo katika Club yake ya Altetico Madrid ya nchini Hispania kwani alisema yeye ni shabiki mkubwa wa Rapper Drake na anatumia uchezaji huu kuonesha heshima kwa Drake.
Aidha pia Antoine Griezmann alisema alikuwa na furaha sana alipoifungia timu yake ya taifa Ufaransa goli la kwanza katika michuano hiyo dhidi ya Albania na hadi ikampelekea asahau kushangilia kwa aina ya ‘HOTLINE BLING’ na alisahau pia kucheza alipofunga goli la kusawazisha dhidi ya Ireland.
Mshambuliaji huyu mwenye magoli 22 katika ligi ya La Liga msimu uliopita atakumbukwa pia kwa kuipeleka timu yake ya Ufaransa katika fainali ya michuano ya Euro baada ya kufunga mara mbili katika ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainal dhidi ya Ujerumani.
- HIT EM FOLKS
Ni aina ya uchezaji ambayo inahusisha kuinyoosha mikono ikiwa katika shepu ikisigana na wakati huo huo unaweza kuunyanyua aidha mguu wa kushoto au kulia. Mara nyingi aina za uchezaji
katika ushangiliaji huwa zinaanzia katika nyimbo alafu wana michezo hukopi lakini imekuwa tofauti kidogo katika aina hii ya uchezaji uitwao ‘HIT EM FOLKS’ kwani imeanzia michezoni ndipo wana muziki wakaichukua.
ODELL BECKHAM Jr
Mchezaji wa mpira wa miguu wa kimarekani wa timu ya New York Giants alionekana akishangilia katika ushindi wa 32-21 dhidi ya Washington Redskins katika uwanja MetLife. Kwa aina hii ya uchezaji huku ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana kwa aina hii ya uchezaji katika ligi ya NFL. Baada ya mchezo kumalizika Odell Beckham Jr, 23, aliulizwa kuhusiana na aina hii ya ushangiliaji na alinukuliwa akisema ni aina ya uchezaji inayoitwa ‘Hit Em Folks’ ni huwa wanaitumia sana katika mji wao wa Atlanta. Baada ya hapo aina hii ya uchezaji ikaanza kujizolea umaarufu na ndipo ikaingia katika muziki, Lil Uzi Vert ni mmoja wa wasanii wanaoitumia sana aina hii ya uchezaji katika nyimbo zake, staa huyo mwenye umri wa miaka 23 kwa sasa anatamba na wimbo wake uitwao ‘Camera’.
- WATCH ME (WHIP NAE NAE)
Watch Me ni wimbo wa kwanza wa Rapper Silento kutoka Atlanta nchini Marekani uliotoka 05/05/2015 Ni wimbo uliofanya vizuri duniani kote hadi kuweza kushika nafasi ya 3 katika chati za muziki za billboard za nyimbo bora 100. Kufanya vizuri kwa huu wimbo uliambatana na aina yake ya uchezaji ya utikisaji miguu na kuutupa mkono moja mbele na mguu ikiwa inaenda tofauti yani kama ukiutupa mkono wa kulia unaambatana na mguu wa kushoto.
MEMPHIS DEPAY
Katika Mchezo wa kufuzu wa ligi ya mabingwa Ulaya baina ya Manchester United na Club Brugge uliomalizika kwa Manchester United kushinda 2-1, Memphis Depay aliweza kuifungia club yake ya Manchester United mabao yote mawili. Baada ya kuifungia club yake goli la pili, mshambuliaji huyo mwenye asili ya Uholanzi alishangia ushindi huo kwa kucheza aina hii ya uchezaji ‘Watch me Whip Nae Nae’.
Instagram @xfowz
Twitter @Fowzwheezy
xfowz@icloud.com