Na Baraka Mbolembole
“Mchezaji Analipwa Kwa Uchezaji wake, anaweza kulazimishwa kwa pesa hata kucheza timu asiyoipenda.
Waamuzi wana utashi binafsi, ila kwa kuwa uamuzi ni “kibarua”, lazima afuate kanuni hata kama zinazamisha jahazi lake.”
“Mpenzi/mshabiki habadilishwi na pesa, Ukiona anahama ujue hata huko anakohamia hana mapenzi nako. Ndio Maana Mpenzi huumizwa au kufurahi zaidi ya mchezaji tokana na kinachotokea Uwanjani.”
“Kuna Maamuzi ya ‘marefa’ ambayo huwa ni kama mafuta ya moto Kwenye nyoyo za mashabiki. Kilichotokea jana Mkwakwani Mwamuzi alijitakia. Coastal si wageni wa kufungwa. Wafunge hata 7, kihalali.
“Wanajikung’uta makalio, wanarejea makwao.” “Upendeleo wa wazi Utakuja kuwatoa roho. Mbona mshika kibendera hakupigwa? Mbona wachezaji pinzani hawakuguswa? Mbona Refa wa akiba hakuguswa? Waamuzi, Mkwakwani Hakuna viti vya kung’oa. “
“Mimi nawalaani wahuni wachache waliompiga refa, Maana atakaa na makovu ya kumbukumbu kwa maisha yake yote. Omar Abubakar ulijitahidi kumuokoa, ukazidiwa, Ramzanee Jr Riwa ulizuia umati mpka ukaangushwa maskini, pole sana.
“Mimi nilikimbia mapema baiskeli yangu isiibwe. Hongera wachezaji kwa kujituma sana.” HAYA NI MAELEZO YA SHUHUDA WA GAME YA Coastal Union v KMC mechi ambayo ilimalizika kwa vurugu kubwa, kisa mwamuzi wa mchezo huo kutoa mkwaju wa penalti kwa timu ya KMC ya Dar es Salaam huku akikataa goli linalodaiwa kuwa halali lililofungwa na Coastal Union.
MTAZAMO WANGU
Mwaka 2005, nikiwa mchezaji wa Eleven Killer pale Morogoro nilifanya tukio la kumpiga kisha kumpokonya kibendera mwamuzi wa pembeni.
Ilikuwa hivi; Timu zote Eleven Killer na wapinzani wetu Chui FC tulikuwa tayari na tiketi ya kucheza ligi daraja la 3 ngazi ya Kanda lakini MRFA-Chama cha Soka Manispaa ya Morogoro walianzisha ligi ya timu nne zilizokuwa zimefuzu kwa ligi ya kanda ili kupata bingwa wa Mkoa.
Chui walikuwa wakihitaji matokeo ya sare tu ili washinde ubingwa na sisi tulihitaji ushindi ili kuwa mabingwa. Katika ligi ya wilaya kila timu haikupoteza mchezo na mechi ambayo tulikutana awali katika ligi ya wilaya ilimalizika kwa sare ya kufungana 1-1.
Mechi ikaanza, dakika ya 6 au ya 7 hivi, tukafungwa goli. Nilimfuata mshika kibendera na kumlalamikia kwamba mfungaji alikuwa katika mazingira ya offside.
Hakunijibu chochote zaidi ya kunyosha kibendera chake kuelekea kati mwa uwanja akimaanisha lilikuwa goli sahihi.
Kama mchezaji nilikuwa na imani kubwa na kikosi chetu na kuamini tungesawazisha na kushinda mechi. Lakini dakika ya kumi tukafungwa goli lingine.
Goli hilo la pili lilifanana na lile la kwanza lakini hili lilinishangaza na kunipandisha hasira zaidi kwa maana mtoaji wa pasi ya goli alipokea mpira akiwa katika mazingira ya offside naye akatoa pasi kwa mwenzake ambaye alikuwa peke yake.
Kwa vile nilikuwa nacheza namba 6, nikakambilia kwa mwamuzi yule wa pembeni. Sikujali uanajeshi wake, baada ya jamaa kufunga goli, nikampiga mtama yule mshika kibendera, ile anainuka akapigwa tena mtama na mchezaji mwenzangu.
Nikaamua kumpora kibendera chake. Nilijua tayari ninakwenda kufungiwa kucheza soka hivyo niliamua kuchukua kibendera kiwe kumbukumbu yangu ya tukio lile.
Mechi ikamalizika dakika ya kumi tu. Hakukuwa na shabiki yeyote aliyeingia uwanjani lakini sisi kama wachezaji tulimuadhibu mwamuzi yule wa pembeni.
Nilifungiwa kucheza soka kwa miezi sita kutokana na tukio lile. Unaweza kuona uchezeshaji mbovu katika game za ligi kuu pekee lakini kiujumla katika soka la Tanzania kuanzia ngazi ya chini mambo si mazuri.
Siamini kama ni pesa au maelekezo pekee wanayopewa waamuzi ili timu fulani ipoteze mechi. Tazama VPL kila kukicha ni matatizo ya waamuzi, tazama Ligi daraja la kwanza kila siku timu zinawalalamikia waamuzi, fuatilia ligi daraja la pili kila mtu analalamikia waamuzi, nenda hadi ligi daraja la 3 na lile la nne pia watu wanawalalamikia waamuzi.
Ni kwanini kila ligi tatizo ni waamuzi? Je, ni kweli wanatumika? Nani anayewatumia? Jambo la kutazamwa hapo ni ufahamu wa sheria za soka.
Kuna waamuzi wengi wanajua kupuliza filimbi, wanajua kukimbia vizuri uwanjani, wanatazama matukio yote lakini amini hawajui sheria 17 za mchezo wa kandanda na kama hawatakubali kujifunza mambo yatazidi kuwa magumu upande wao.
Haiwezekani kila ligi waamuzi wakawa wabovu! Haiwezekani kuwa kila mwamuzi anayeboronga awe amenunuliwa! Haiwezekani kila mwamuzi akoseapo atakuwa na mapenzi binafsi dhidi ya timu nyingine! Nachokiona ni upeo wao mdogo kuhusu ufahamu wa sheria za kandanda na jinsi ya kuzisimamia si kingine.
Waamuzi ni tatizo lakini shabiki hapaswi kumpiga mwamuzi. Ukitazama vizuri video ya tukio la jana katika game ya Coastal v KMC utamuona askari polisi anavyo pambana kumuokoa mwamuzi kumtoa uwanjani kumnusuru na kipigo. Je, hivyo ndivyo ivyopaswa kufanyika?