
Yusuf Manji, Mwenyekiti wa club ya Yanga na mgombea udiwani kata ya Mbagala Kuu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM)
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Yusuf Manji amesema suala la kuchelewa kujengwa kwa uwanja wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kuongezewa eneo ndio kumechochea yeye kuamua kugombea nafasi ya Udiwani ili iwe rahisi kupigania kibali hicho.
Manji ameongeza kuwa, suala la kuwa na uwanja wa mazoezi kwake sio kitu kikubwa kwasababu kutumia milioni 200 kujenga uwanja wa mazoezi wakati wanatumia zaidi ya milioni 30 kwa msimu kwa ajili ya kukodi viwanja kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Shaffihdauda.com: Ni kitu gani ambacho unajivunia tangu uingie kwenye uongozi wa klabu ya Yanga kama mwenyekiti ambapo kwa sasa muda wako wa kukaa madarakani unaelekea ukingoni?
Manji: Nimeweza kurudisha imani ya wapenzi wa Yanga kwa timu yao na viongozi wao, sikuhizi hakuna kelele kama ilivyokuwa zamani, tukifungwa ni mpira na tukishinda ni mpira tunalia na kufurahi pamoja bila kulaumiana wenyewe kwa wenyewe.
Hicho ni kitu kikubwa ambacho najivunia japo sijafanya pekeangu, ni uongozi mzima pamoja na mashabiki tunashirikiana pamoja.
Shaffihdauda.com: Mliomba kuongezewa eneo la Jangwani kwa ajili ya kujenga uwanja wa klabu ya Yanga, lakini mpaka sasahivi hakuna kilichofanyika juu ya uwanja. Mpango wenu wa kujenga uwanja huo bado upo?
Manji: Moja ya sababu zangu za kuamua kugombea Udiwani ni pamoja na hilo. Maamuzi mengi lazima yafanywe na wakubwa, lakini maamuzi ya kwenye halmashauri yanafanywa na madiwani, madiwani wanaweza kuamua kwenye ngazi ya halmashari kwa kusema ndiyo au siyo.
Mimi sioni kama kuna haja ya klabu kama Yanga au Simba kwenda porini kujenga uwanja wa mpira. Timu kama Real Madrid, Manchester United, Liverpool, Barcelona zote zipo mjini, na wamejenga viwanja mijini ili mashabiki wajae, lakini ukienda porini mashabiki watakuwa hawajai kwasababu hapafikiki kirahisi. Dhamira Yangu bado nataka uwanja ujengwe mjini.
Shaffihdauda.com: Umeamua kuwania Udiwani, hii inamaanisha utaachana na Yanga moja kwa moja au utaendelea kuwepo kwenye klabu ya Yanga hata kama ukichaguliwa kuwa diwani?
Manji: Nafasi ya uwenyekiti wa Yanga ni nafasi ambayo nimechaguliwa hivi karibuni tu miaka miwili au mitatu iliyopita. Kabla ya hapo nilikuwepo Yanga, mimi sitafuti cheo, natafuta maendeleo. Naweza kuchangia maendeleo ya Yanga nikiwa kwenye nafasi yoyote ile, nilianza nikiwa kama mwanachama, sasahivi mwenyekiti na hata kiacha nafasi hii nikaingia nafasi nyingine bado naweza kusaidia maendeleo ya Yanga.
Shaffihdauda.com: Suala la uchaguzi wa viongozi wa Yanga limechelewa na sasahivi viongozi waliopo madarakani wanafanya kazi huku muda wao ukiwa umemalizika, watu wanataka kujua nini kimesababisha uchaguzi kuchelewa kufanyika hadi leo?
Manji: Kwanza suala la uchaguzi halipo chini yangu bali suala hili lipo chini ya kamati ya uchaguzi. Kuna kamati tatu ambazo mimi sina mamlaka ya kuziondoa, kamati ya maadili, kamati ya uchaguzi na kamati ya nidhamu mimi siwezi kuwalazimisha kutangaza tarehe ya uchaguzi.
Jambo la pili ni katiba ambayo TFF waliagiza ifanyiwe mabadiliko na muda wa kufanya hivyo umekuwa hautoshi kwasababu ili urekebishe katiba inabidi ukutane na wanachama kwa hiyo nayo ni changamoto.
Viongozi wengi wa mpira wanaingia kuongoza mpiraili wapate sehemu ya kufanya mambo yao mengine kama siasa na biashara, lakini kitu kingine ni kwamba ligi yetu haijawa ‘stable’ bado timu zinazocheza ligi ni chache ukilinganisha na ligi nyingine zenye timu 18 hadi 20 ambapo wachezaji wanaweza kupata michezo mingi.
Shaffihdauda.com: Uwekezaji kwenye soka la vijana ukoje kwenye klabu ya Yanga?
Manji: Tumewekeza lakini wapenzi wa mpira wao kila siku wanataka ushindi, huwezi kusema nitawekeza kwenye timu ya vijana tusubiri baada ya miaka 10 ndio tuchukue ubingwa. Lakini hii ni changamoto kwa timu zote duniani, kipindi cha usajili unakuta timu inasajili wachezaji 8 hadi 9 kutoka nje wakati ina Academy.
Academy inanafasi katika kupunguza gharama lakini sio kipaumbele changu, mimi naanza na timu ya wakubwa, halafu uwanja na academy inafata baadae.