
Mshambuliaji wa Goms United akiwa amebebwa juu na mashabiki wa timu yake baada ya kufunga goli la tatu dhidi ya Kauzu FC na kuzima ndoto za Kauzu kusonga mbele kwenye michuano ya Magufuli Cup
Timu ya Goms United kutoka Gongolamboto imeitupa nje timu ya Kauzu FC ‘Wauzu mitumba’ wa Tandika kwa ushindi mnono wa wastani wa goli 4-1. Mchezo uliopigwa leo kwenye uwanja wa Bandari, Temeke umemalizika kwa Goms United kuichapa Kauzu FC kwa goli 3-1.
Magoli ya Goms United yamefungwa na Samboni Nacho dakika ya 50, Ema Pius dakika ya 64 na Haji Zege dakika ya 85 wakati goli pekee la Kauzu FC limewekwa wavuni na Ally Kalulu dakika ya 81.
Mchezo wa awali uliopigwa kwenye uwanja wa Kampala, Gongolamboto, Goms United ilipata ushindi wa nyumbani wa goli 1-0 dhidi ya Kauzu FC kabla ya leo kushusha kipigo cha kutosha wakati Kauzu wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Bandari.
Ushindi huo unaifanya Goms kuwa timu ya tatu kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano ya Maufuli Cup #Hapa Kazi Tu ikisubiri mshindi wa mechi kati ya Faru Jeuri dhidi ya Friends Rangers.
Kesho michuano ya Magufuli Cup itaendelea tena kwa mchezo mmoja kupigwa kati ya Faru Jeuri dhidi ya Friends Rangers mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Bandari, Tandika, Temeke.