Jumatatu November 14, picha za beki wa kati wa Azam FC Pascal Wawa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha nyota huyo raia wa Ivory Coast akisaini mkataba wa kurejea kwenye timu yake ya zamani Al-Merrikh Sporting Club ya nchini Sudan aliyoitumikia kwa miaka minne kabla ya kujiunga na Azam mwishoni mwa mwaka 2014.
Kipindi cha Mshikemshike Viwanjani kinachorusha na Azam TV kimemnukuu Wawa akithibitisha kusaini mkataba wa awali wa kujiunga na Al-Merrikh huku akitoa sababu kadhaa zilizomfanya kufikia uamuzi wa kuachana na Azam FC.
“Sijasaini mkataba wenyewe, nimesaini mkataba wa awali haukuwa mkataba kamili,” amesema mlinzi huyo aliyejizolea umaarufu kwenye michuano ya Kagame 2015 kwa kuiongoza safu ya ulinzi kucheza mechi zote za mashindano hayo bila kuruhusu goli ndani ya dakika 90 na kuipa Azam ubingwa wa taji hilo kwa mara ya kwanza.
“Nilipata majeraha hapa, bosi Yusuf pekee ndiye aliyenisaidia sana lakini baada ya majeraha hakuna hata mmoja aliyeongea na mimi kuhusu mkataba wangu, nilichanganyikiwa nikawa sijui kama nitabaki hapa au nitaenda sehemu nyingine.”
“Nilienda Nairobi kuitafutia familia yangu visa kwasababu nataka kwenda Ufaransa kwa mapumziko, Al-Merrikh wakanipigia simu. Tulianza kuwasiliana kwa Whatsapp halafu wakanipa ofa nzuri nikakubali kwasababu niliwasubiri sana Azam lakini hakuna aliyeongea na mimi basi nikaamua kusaini mkataba wa awali, nitaenda kwanza nchini kwangu na familia yangu baada ya mapumziko naweza kusaini.”
Mtendaji mkuu wa Azam FC Saad Kawemba amesema ameomba taarifa za Al Mereikh kutaka kumsajili Wawa ili uongozi wa klabu ya Azam FC uweze kuzifanyia kazi.
“Wenzetu wa Al-Merrikh walinipigia simu jana jioni wakathibitisha kwamba wanania ya kumsajili Wawa na wanaelewa kwamba mkataba wake unaisha kwahiyo wanahitaji kufanya nae kazi. Nikawaambia tunapenda kuona taarifa zao ili tuweze kuzifanyia kazi, kwahiyo wameahidi kututumia kwenye klabu yetu hizo taarifa zote.”
“Kitu muhimu ni kwamba, mchezaji alikuwa Sudan jana katika moja ya mazungumzo ya ile jioni na ni moja ya watu ambao niliongea nao. Sasahivi yupo nchini tutapata nafasi ya kuzungumza nae, ni mchezaji wetu na tunaamini ni mtu mzima sio mtoto mdogo kwahiyo atakuwa na la kutueleza.
Pascal Wawa hajacheza kwenye kikosi cha Azam FC tangu alipopata majeraha wakati wa mchezo wa hatua ya pili wa mashindano ya kombe la shirikisho Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia April 10 mwaka huu mchezo ambao Azam walishinda kwa bao 2-1.