Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Nje ya pitch: Ni wakati wa Azam kutathimini upi mfumo sahihi wa kujenga timu

$
0
0

img_0004

Na Athumani Adam

Juzi kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya benchi la ufundi la klabu ya Azam liliendesha majaribio na hatimaye kuwapata wachezaji kumi ambao wataungana na wengine hamsini kutoka mikoa mingine kwa ajili ya mchujo wa mwisho utakaofanyika Dar es salaam mwezi Desemba mwaka huu.

Vijana wataofuzu kwenye majaribio ya mwisho watajiunga na timu za vijana chini ya umri wa miaka kumi na saba ya klabu hiyo.

Wakati majaribio ya kutafuta vijana wenye uwezo kuichezea Azam chini ya umri wa miaka kumi na saba yakiendelea, washambuliaji wawili raia wa Ghana Samuel Afful pamoja na Yahya Mohamed wamesajiliwa kwenye dirisha dogo. Bila shaka kufanya vibaya kwa safu ya ushambuliaji ya Azam ndio sababu ya kuwaongeza ‘maproo’ hao.

Azam imekuwa haina makali kwenye idara ya ushambuliaji tangu kuanza kwa msimu wa ligi kuu Tanzania bara 2016/17.  Baada ya kumalizika msimu wa ligi 2015/16 Azam iliiachana na washambuliaji wa kimataifa Muivory Coast Kipre Tchetche aliyenda nchini Oman.

Pia wakaachana na washambuliaji   Allan Wanga na Didier Kavumbagu huku nafasi zao zikichukuliwa Muivory Coast mwingine  Gonazo Bi Ya Thomas na Mghana Enock Agyei.

Si Ya Thomas wala Enock Agyei ambao wamefanya vizuri kwenye msimu huu wa ligi wakiwa na klabu ya Azam. Wote wawili hawana mabao ya kutosha japokuwa wanacheza kwenye idara ya ushambuliaji.

Kifupi Azam wanaonekana kukosea wakati wa dirisha kubwa la usajili, lakini bado wanatumia njia zile zile kujaribu kusafisha makosa yaliyotokea wakati wa usajili uliopita. wanaendelea kuamini katika kutumia wachezaji wa kimataifa kama ilivyozoeleka kwenye vilabu vingi barani Afrika.

Lakini wanapaswa kujiuliza kama unaleta washambuliji watatu kutoka nje ya nchi halafu wakashindwa kufanya vizuri nini tatizo? Kina Allan Wanga walishindwa msimu uliopita kama ambavyo kina Ya Thomas wanavyoelekea kushindwa msimu huu.

Sina hakika hawa Waghana walioletwa hivi karibuni kipi watafanya kwenye mzunguko wa pili wa ligi. Takwimu zinawabeba huko walipotoka lakini hata Ya Thomas alikuja kwenye ligi ya Vodacom akiwa na takwimu nzuri.

Kwa Tanzania hakuna timu yenye mifumo mizuri ya soka la vijana kama Azam. Nadhani huu ulikuwa ni wakati sahihi kwao kuwatumia vijana wanaotengenezwa pale Chamanzi huku wakitumia wachezaji wachache kutoka nje.

Kama kina Farid Mussa, Aishi Manula, Himid Mao na wengine wameweza kufanya vizuri kwa kutoa mchango mkubwa kwenye timu kwanini kila mwaka waendelee kutafuta maproo kutoka nje.

Timu za Afrika Kaskazini zinapata mafanikio kila siku kwenye soka la Afrika kupitia wachezaji wao vijana wa ndani. Tunisia, Misri, Morocco na Algeria vilabu vyao vinachukuwa proo mwenye vitu vya ziada. Bahati mbaya kwa Tanzania timu zetu zina sajili kujaza nafasi saba  za wachezaji wa kigeni.

Timu kama Mo Bejaia ambayo ilikuwa kundi mmoja na Yanga kwenye mashindano ya shirikisho imefanya vizuri hali ya kuwa ina wachezaji kutoka nje ya Algeria wasiozidi watano.

Kwenye soka la siku hizi kuna mifumo miwili ya kutengeneza timu, kwanza ni kununua wachezaji waliokamilika pili ni kutengeneza vijana na kuja kuwatumia baadae. Bahati nzuri Azam ina mifumo yote miwili lakini mfumo wa kwanza unaonekana kusumbua kwa siku za karibuni.

Imekuwa ngumu kuziba pengo la Kipre Tchetche kama ambavyo itakuwa ngumu kumpata mrithi wa Pascal Wawa aliyeondoka kwenye dirisha dogo la usajili. Nadhani njia sahihi ni kuanza kuwatumia kina Shabani Idd vijana waliopitia mifumo ya soka la vijana. Kina Idd wana uwezo mkubwa kuliko baadhi ya maproo waliopo kwenye timu zetu.

Wakati majaribio ya kusaka vijana yakiendelea ni wakati sahihi kwa Azam kujithimini juu ya mifumo yake ya kujenga timu. Kwa upande wangu nadhani vijana wana tija zaidi kuliko mastaa kutoka Afrika Magharibi. Mtazame mara mbili Farid Mussa utakubaliana na nachokisema.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles