Nyota wa Barcelona Neymar jana alifunga mabao manne wakati Barcelona ilipopata ushindi wa goli 5-2 mbele ya Rayo Vallecano kwenye mchezo wa ligi kuu ya Hispania (La Liga).
Rayo Vallecano ndio walikuwa kwanza kufunga goli la kwanza kupitia kwa Guerra dakika ya 15 kipindi cha kwanza.
Dakika ya 22 Neymar alisawazisha goli hilo kwa mkwaju wa penati baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari, Neymar alifunga goli la pili kwa mkwaju wa penati pia kufuatia kuangushwa tena kwenye eneo la hatari.
Haikuishia hapo, dakika ya 69 Neymar alifunga goli la tatu na kujiandikia Hat-trick kwenye mchezo huo kabla ya kutundika goli la nne dakika moja baadae na kufanikiwa kufunga magoli manne kwenye mechi hiyo.
Luis Suarez alikamilisha ushindi wa goli 5-2 wa Barcelona baada ya kupachika goli dakika ya 77.
Jozabed aliifungia Vallecano goli la pili zikiwa zimesalia dakika nne mchezo huo kumalizika.
Hapa chini unaweza kuangalia video ya magoli yote yaliyofungwa kwenye mchezo huo.