Ushindi wa 1-0 dhidi ya African Sports, kisha 2-0 dhidi ya JKT Mgambo katika michezo miwili ya ufunguzi waliyocheza Mkwakwani Stadium, Tanga ulikuwa ni ‘mwanzo usiotarajiwa’ wa kikosi cha Simba SC msimu huu. Si kwa kucheza mpira wa kuvutia sana, bali Simba chini ya kocha Muingereza, Dylan Kerr ilicheza mchezo wa kusaka matokeo ya ushindi zaidi na wakafanikiwa kushinda mara mbili mfululizo ndani ya siku nne.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Dar es Salaam kushinda katika uwanja wa Mkwakwani baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu mitatu iliyopita. Ushindi wa 3-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa raundi ya tatu ulikuwa ni kwanza pia kwa ‘ Wekundu wa Msimbazi’ dhidi ya timu hiyo ya Kagera katika uwanja wa Taifa.
Kufikia raundi ya tatu msimu huu kikosi cha Kerr kilikuwa kimeweza kuvunja mwiko wa misimu mitatu mfululizo. Simba ilishinda kwa mara ya kwanza Mkwakwani baada ya kusubiri kwa misimu mitatu, pia ikaifunga Kagera Sugar kwa mara kwanza Kagera Sugar katika uwanja wa Taifa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu mitatu iliyopita.
Wakachapwa 2-0 na mahasimu wao Yanga SC katika mchezo wa raundi ya nne. Wakicheza soko la kiwango cha chini wakaishinda 1-0 Stand United. Ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa Simba dhidi ya timu hiyo ya Shinyanga ambayo ilipanda ligi kuu msimu uliopita.
Kerr amekuwa akisifia uchezaji wa timu yake licha ya kwamba katika mazingira ya kawaida timu yake haichezi vizuri. Safu yake ya ulinzi imekuwa makini sana, licha ya kuruhusu magoli matatu uchezaji wa Hassan Kessy na Mohamed Hussein katika fullbacks umekuwa si mzuri sana.
Wachezaji hao wamekuwa wakipanda kwa wakati mmoja jambo ambalo lilikaribia kuwagharimu katika mchezo wa ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City FC siku ya Jumamosi iliyopita. Juuko Murishid, Justice Majabvi naweza kuwataja kama wachezaji ‘mihimili’ ya Simba hivi sasa.
Wamekuwa wakijaribu ‘kufuta’ makosa mengi ya walinzi wa pembeni, wanacheza kwa nguvu na moyo wa kuhitaji ushindi tu hivyo hawako tayari kufanya makosa rahisi. Majabvi alifunga goli la kuongoza katika ushindi dhidi ya Mgambo, wakati Murishid alifunga goli pekee katika ushindi dhidi ya City.
Simba ilicheza vizuri kwa dakika 15 tu katika mchezo uliopita lakini wakaendelea kupata ushindi wa 100% katika gemu za ugenini msimu huu. Wamevunja mwiko mwingine wa kutoishinda City katika ligi kuu baada ya kushindwa kufanya hivo kwa misimu miwili iliyopita.
Ushangiliaji wao wa ‘stahili ya kujipipa picha-selfie’ huku wakiwa katika mstali mmoja ulivutia kwa hakika lakini hali hiyo itaendelea dhidi ya Tanzania Prisons timu ambayo wameishinda mara mbili tu katika uwanja wa Sokoine, Mbeya katika miaka 15 hii?.
Prisons ni moja ya timu ngumu kufungika katika uwanja wa nyumbani ikicheza na Simba. Ilipoteza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11 dhidi ya Simba msimu wa 2008/09 pia walipoteza nyumbani msimu wa 2012/13. Chini ya kocha Salum Mayanga, Prisons imekuwa na matokeo ya kupanda na kushuka kwani imechapwa mara tatu katika michezo 7 msimu huu.
Imeshinda mara tatu, mara mbili nyumbani huku ushindi wao mkubwa msimu huu ukiwa ule wa ugenini dhidi ya Kagera Sugar (walishinda 3-0), walipoteza gemu iliyopita dhidi ya Stand United ugenini.
Ally Manzi na Jeremiah Juma wamefunga magoli manne kati ya 6 ya Prisons na washambuaji hao wawili hawakufunga katika kichapo kizito walichopata Kambarage Stadium, Shinyanga mbele ya wenyeji Stand United ambapo vijana wa Mayanga walipigwa 3-0 na kufikisha magoli 8 ya kufungwa. Richard Peter anaweza kucheza mchezo wa Jumatano na mfungaji huyo namba moja wa Prisons si wa kumletea masihara hata kidogo.
Nahodha wa Simba, Musa Hassa hajafunga goli lolote katika gemu 5 alizopewa nafasi, na katika magoli 8 waliyofunga Simba ni mchezaji mmoja tu wa nafasi ya mashambulizi aliyefunga hadi sasa, Mganda Hamis Kiiza ambaye ametupia kambani mara 5. Ili kuishinda Prisons ni lazima Simba wapandishe kiwango chao na kuongeza jitihada katika safu ya mashambulizi. Wanacheza vizuri katikati kwa kuwa wanapangwa viungo wengi ila si timu imara katika eneo hilo.