Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Bushiri si chaguo sahihi lakini anaweza kuwa bora Mwadui FC

$
0
0

Mwadui FC

Na Baraka Mbolembole

CHAGUO la Ally Bushiri kama kocha wa Mwadui FC si baya, lakini nadhani timu hiyo ilihitaji kocha bora na mwenye uzoefu zaidi katika soka la Tanzania Bara ili waepuke kushuka daraja msimu huu.

Ni kweli kuna tofauti ya pointi chache kati ya Mwadui FC iliyo nafasi ya 15 katika msimamo wa timu 16 na timu zilizo juu yao. Ndanda FC iliyo nafasi ya kumi imekusanya alama 19, pointi 6 zaidi ya Mwadui iliyo nafasi ya pili kutoka chini ya msimamo.

Bushiri amewahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Zanzibar wakati wa utawala wa Mbrazil, Marcio Maximo, pia ni kocha mwenye mafanikio katika soka la Zanzibar lakini Mwadui itakuwa imecheza ‘kamari’ ambayo inaweza kuwarejesha ligi daraja la kwanza.

Mwadui wana kikosi kizuri chenye wachezaji wazoefu wa ligi na chipukizi wenye uwezo mzuri ndani ya uwanja.

Paul Nonga, Jerson Tegete, Abdallah Seseme, nahodha Shaaban Kado, Kabunda, Joram Mvegeke ni baadhi ya wachezaji waliopo katika timu hiyo ya Shinyanga ambayo ilishinda michezo mitatu tu na kupoteza 8, huku wakipata sare nne katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.

Kuna wakati makocha bora kutoka Zanzibar miaka ya hivi karibuni, Salum Bausi aliyekuwa akiifundisha African Lyon na Hemed Morocco aliyekuwa Coastal Union ya Tanga walipata kufundisha timu hizo katika VPL msimu wa 2013/14 lakini wakaishia kuuponda mpira wa Bara huku wakilalamika sana kuhusu waamuzi na viongozi wa timu zao.

Sijapendezwa na chaguo la Bushiri kama mrithi wa Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ katika timu ya Mwadui FC. Kwa aina ya wachezaji waliopo katika timu hiyo, Suleimani Matola, Mbwana Makata na kuna wakati nilisema Bakari Shime-mmoja kati ya makocha hawa angewafaa zaidi Mwadui kuwaondoa katika eneo hatarishi walilopo katika msimamo wa ligi.

Hawa ni makocha wazuri, pia ni makocha ambao wanaweza kufahamu na kujua jinsi ya kuwatumia wachezaji ili kuepuka kushuka daraja. Bushiri alikuwa kipa mahiri wakati wake wa uchezaji, hilo pia linaweza kumfanya kushindwa kuisaidia timu yake ya sasa kimbinu.

Anachopaswa kufanya sasa kwanza ni kuongeza hamasa katika kikosi chake na kuwaambia wachezaji wake wanaweza kumaliza juu ya nafasi kumi za juu. Wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kupewa mbinu za kutafuta nafasi na kufunga magoli. Naamini Bushiri ataimarisha ngome yake iliyoruhusu magoli 21 katika mzunguko wa kwanza kwa sababu eneo hilo analifahamu vizuri na ana mbinu nzuri za kujilinda.

Wachezaji wa Mwadui wanapaswa kuamka na kupambana kuhakikisha wanashinda vita ya kutoshuka daraja misimu miwili baada ya timu hiyo kupandishwa na Julio.

Bushiri si chaguo sahihi lakini linaweza kuwa bora Mwadui FC kama watashirikiana, huku pia wachezaji wakichukua mafunzo yake na kuzitumia mbinu zake.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>