Na Baraka Mbolembole
LIGI Kuu ya kandanda Tanzania Bara inataraji kuendelea tena wikendi hii baada ya mwezi mmoja wa mapumziko uliombatana na usajili wa dirisha dogo.
Mbeya City FC itacheza na Kagera Sugar FC siku ya Jumamosi katika uwanja wa Sokoine, Mbeya. Mkufunzi wa timu hiyo, Mmalawi, Kinnah Phiri ameongeza nguvu katika kikosi kilicho nafasi ya nane baada ya kukusanya alama 19 katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.
Phiri-kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Malawi ameongeza wachezaji sita wapya kikosini mwake huku wanne kati yao wakitoka nje ya Tanzania.
Timu hiyo ya ‘kizazi kipya’ imempoteza kiungo wake mshambuliaji Joseph Mahundi aliyemaliza mkataba na kujiunga na Azam FC.
Raia wa Uganda, Hood Mayanja, Titto Okello na William Otong wamejiunga na timu hiyo wakitokea African Lyon ya Dar es Salaam, mshambulizi Mzimbabwe, Tsipa Leonard.
Kwa mara ya kwanza timu hiyo ya Mbeya imesajili wachezaji 7 wa kigeni, awali walikuwepo Owone Chaina golikipa raia wa Malawi, Hemed Murutabose raia wa Burundi na mlinzi imara wa kati kutoka Malawi, Sankhan Mkandawile.
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam FC, JKT Ruvu na Simba SC, Zahoro Pazzi amesajiliwa
kikosini humo kama mbadala wa Mahundi sambamba na Juma Seif Kijiko.
Hussein Dotto pia amejiunga na timu hiyo katika usajili huu akitokea Stand United ya Shinyanga. Usajili huu unaweza kuisaidia City timu iliyopanda daraja mwaka 2013.