Msanii maarufu wa Bongo Movies Jacob Steven ‘JB’ amesema Simba kuifunga Yanga si jambo la ajabu na itaendelea kufungwa kila itakapokutana na mnyama.
JB ambaye ni shabiki wa kutupwa wa Simba alikuwepo uwanja wa Amaan mjini Unguja kuishuhudia timu yake wakati ikipambana na Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe la Mapinduzi.
“Si ajabu Yanga kufungwa na Simba, ni kitu cha kawaida na wataendelea kufungwa tu. Tukitoka kwenye mashindano haya tunarudi Dar ambako tutakutana tena kwenye ligi huko pia wasubiri kichapo kingine,” anasema JB ambaye alishuhudia mchezo akiwa amekaa chini kwa dakika zote 90.
JB alikuwa mtulivu akifatilia kwa makini mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda kwa penati 4-2.
January 13 siku ya Ijumaa, Simba itacheza na Azam FC mchezo wa fainali kutafuta bingwa mpya wa michuano ya 11 ya Mapinzuzi kwa mwaka 2017.