Na Abubakar Khatib ‘Kisandu’, Zanzibar
Suleiman Ali ‘Pishori’ ambae kwasasa ni mchezaji wa Kilimani City akitokea Miembeni katika dirisha dogo la usajili ndiye mchezaji anayeongoza kucheza mara nyingi kuliko mchezaji yoyote kwenye Mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo yanahitimishwa usiku wa leo kwenye fainali kati ya Simba dhidi ya Azam FC.
Pishori amecheza jumla ya mechi 24 katika mashindano hayo akiwa na timu nne tofauti tangu mwaka 2007 yalipoanzishwa mpaka 2014 alipoishia kucheza hivyo amecheza miaka 8 mfululizo pasipo kupumzika na ndio mchezaji mwenye historia kubwa ya kucheza Mashindano hayo mara nyingi zaidi.
Alianza kucheza mwaka wa kwanza lilipoanzishwa kombe hilo ilikuwa mwaka 2007 akiwa ni mchezaji wa Jamhuri akicheza nafasi ya mlinzi wa kushoto ambapo hapo Jamhuri alicheza mara tatu mfululizo yani mwaka 2007 hadi 2009.
Msimu uliofuata alihama Jamhuri ya Wete Kisiwani Pemba na kuhamia timu ya Ocean View ambapo ulikuwa mwaka 2010 na pia mwaka huo akacheza kombe hilo la Mapinduzi ikiwa ni mwaka wake wa 4 mfululizo.
Mwaka 2011 pia akacheza tena na timu hiyo ya Ocean View ikawa ni mwaka wake wa tano mfululizo.
Msimu mwingine akahama Ocean View na kujiunga na timu ya Miembeni ‘Wazee wa Kwalalumpa’ ambapo ilikuwa ni mwaka 2012 na pia timu hiyo alicheza mara mbili mfululizo yani mwaka huo 2012 na mwaka 2013 na pia ilikuwa ni mwaka wake wa 7 kucheza na kombe hilo.
Msimu wake wa mwisho kucheza kombe hilo Pishori ilikuwa ni mwaka 2014 ambapo alikuwa ni Nahodha wa timu ya Kombain ya Unguja ilikuwa inajulikanwa kwa jina la Spice Stars.
Mtandao huu umezungumza nae kutaka kujua anajisikiaje kuwa ndio mchezaji aliecheza mara nyingi Michuano hiyo ambapo amefurahi sana kuweka rekodi hiyo.
“Unajua mimi mwenyewe sijategemea kama ntakuwa nimeweka rekodi hii, najisikia furaha mashindano ya Mapinduzi ni ya Zanzibar na mimi niliyeweka rekodi hii ni Mzanzibar, nafurahi sana kuona na mimi nimeweka rekodi kubwa kama hii, japo sijachukua taji lakini nilifika fainali mwaka 2010 tukafungwa Ocean View 0-1 Mtibwa kule Gombani Pemba, lakini naamini nitaendelea kucheza tena Mashindano haya kwa vile bado naendelea kucheza soka, unajua hili kombe kubwa sana angalia hamasa yake lazima ujivunie kwa hili,” alisema Pishori.