Nicasius N Agwanda (Nicasius Coutinho Suso)
Mashabiki wa klabu ya Los Angeles Lakers na mchezaji Kobe Bryant au The Black Mamba, sasa wanaweza kuwa na ahueni baada ya taarifa rasmi kutoka kuwa mchezaji huyo atakuwepo katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya klabu ya Minnesota Timberwolves siku ya Jumatano. Awali ilizua hofu kwa mashabiki wengi wa Lakers baada ya Kobe Bryant mwenye umri wa miaka 37 kuumia mguu wake katika mchezo wa maandalizi tarehe 13.
Tangu hapo Kobe Bryant hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari ingawa kocha wake Scott Brown alikaririwa akisema sio majeraha makubwa na anaamini kuwa Kobe Bryant atarejea siku ya mechi yao ya ufunguzi ya ligi ya NBA msimu huu siku ya Jumatano.
Jambo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa klabu ya Lakers ni kuona kama mchezaji huyo anaweza kuwarejeshea heshima na nguvu ya kuwa washindani msimu huu, ukizingatia ugumu wa kanda ya magharibi ambayo vilabu vyake vingi vina uwekezaji wa khali ya juu na vipaji vingi sana.
Katika misimu miwili iliyopita Kobe amekuwa akikumbwa na majeraha yanayojirudia rudia na wataalamu wengi na wachambuzi mbalimbali wakisema kuwa umri wake kwa kiasi kikubwa unachangia sana mwili wake kuchoka na kupata majeruhi ya mara kwa mara. Swali linabaki je, Kobe atakuwa fiti msimu mzima, na je atakubali kupunguziwa majukumu uwanjani na dakika? Kobe ni Lakers na Lakers ni Kobe.
Mchezaji veterani wa klabu hiyo ametamka kuwa katika mazoezi ya siku ya Jumapili, Kobe alirejea kwa mara ya kwanza katika mazoezi ya pamoja na alionekana kuwa fiti sana kiasi kwamba mitupo yake ilikuwa sawia na kila alichofanya kilionekana kuwa vyema sana.
Kobe anaingia katika msimu wake wa 20 na klabu ya Los Angeles Lakers ambao pia ni wa mwisho katika mkataba wake, huku akiingiza pesa nono zaidi ambayo ni dola za kimarekani milioni 25 ($25 million).