Na Zainab Rajab
Timu ya Azam imefanikiwa kuingia kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup au FA Cup baada ya kuibuka na ushindi wa goli 3-1 dhidi ya Cosmo Politan inayoshiriki ligu daraja la pili.
Ilichukua muda kwa Azam kuandika goli la kwanza ambapo golikipa wa Cosmo alimbabatiza John Bocco na mpira ndani ya 18 na kurudi golini.
Haikuchukua muda sana Shaban Idd akatumia pasi safi iliyopigwa na John Bocco ikiwa ni uzembe pia wa golikipa na kuiandikia Azam goli la pili, Cosmo wakiendelea kujitutumua angalau kurejesha matumaini kwa kikosi chao Fidelisi Kyangu anaipatia timu yake goli la kufutia machozi akiunganisha mpira wa kona.
Joseph Mahundi akiwa peke yake aliweza kuiandikia Azam goli la tatu na la ushindi na kuzima kabisa matumaini ya Cosmo.
Baada ya matokeo hayo, Azam wanaungana na timu nyingine zilizofanikiwa kushinda kwenye michezo yao iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii kusonga mbele kwenye michuano hiyo.