
Mshambuliaji kinda wa Simba Ibrahim Ajib amefanikiwa kufunga hat-trick wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa goli 6-1 dhidi ya Majimaji FC ya Songea kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliochezwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Ajib alianza kufunga goli la kwanza dakika ya nane (8) ya kipindi cha kwanza akiunganisha pasi iliyopigwa na mlinzi wa kulia wa timu hiyo Emery Nimubona baada ya kumtoka Ally Mohamed mlinzi wa kushoto wa Majimaji FC.
Mambo bado yaliendelea kumnyookea Ajib kwani dakika sita baadae alipachika bao la pili akiunganisha krosi iliyopigwa na Mohamed Hussein Tshabalala. Goli hilo liliamsha kasi ya Ajibu kuanza kuitafuta hat-trick kwa uchu.
Ndoto za Ajib kufunga goli tatu kwenye mchezo huo zilitimia dakika ya 42 kipindi cha kwanza baada ya kufanikiwa kufunga goli la tatu na kujihakikishia kuondoka na pira.
Hiyo imekuwa ni hat-trick ya tatu kwa Ajib akiwa Simba lakini ni ya pili kwake kwenye ligi kuu ya Vodacom. Ajib alifunga hat-trick yake ya kwanza kwenye michuano ya Mapinduzi Cup Zanzibar kisha akapiga hat-trick nyingine kwenye ligi kuu msimu uliopita huku akipiga goli tatu nyingine kwenye mchezo wa ligi kuu msimu huu dhidi ya Majimaji.
Hat-trick hiyo ni ya pili kwenye ligi kuu ya Vodacom msimu huu baada ya Kiiza kufunga hat-trick ya kwanza msimu huu wakati Simba ilipocheza dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa taifa.