
Hatimaye timu ya maafande wa JKT Ruvu leo imepata ushindi wake wa kwanza tangu kuanza kwa ligi kuu ya Vodacom msimu huu, JKT Ruvu ilicheza michezo tisa bila kupata ushindi lakini leo imeweza kuchukua pointi tatu ikiwa ugenini kwa ushindi wa goli 2-0 dhidi ya African Sports.
Goli la kwanza la Ruvu limefungwa dakika ya 19 kipindi cha kwanza na Musa Juma Kimbu wakati goli la pili limefungwa dakika ya 90+ mfungaji akiwa ni Samwel Kamuntu.
Ushindi huo unaifanya JKT Ruvu kukimbia kutoka mkiani mwa ligi na kusogea hadi nafasi ya 14 ikiwa na pointi tano baada ya kucheza michezo 10 huku Africans Sports ikishuka na kushikilia mkia wa ligi hiyo ikiwa na pointi tatu.
Mchezo mwingine wa ligi ulichezwa jijini Mbeya kwenye uwanja wa Sokoine kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Ndanda FC, mchezo huo umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana kwa magoli 2-2.