Michuano ya Azam Federation Cup imeendelea kwenye manispaa ya Songea kwa kuzikutanisha The Might Elephant ya songea na African Wanderers ya Iringa. Mchezo huo uliopigwa katika dimba la Majimaji mjini Songea, The Might Elephant wakiwa wenyeji wa African Wanderers kutoka Iringa.
Mtanange huo ulianza kwa timu zote kuwa na lengo la kuibuka na pointi tatu muhimu ili kupata nafasi ya kusonga mbele katika hatua nyingine ya mashindano hayo, The Might Elephant ilitawala vyema mchezo huo lakini hawakuweza kutumia nafasi tele walizozipata.
Mpaka kipyenga cha mwisho cha mwamuzi Rajabu Mrope kutoka Songea, timu hizo zilikuwa sare ya bila kufungana na hivyo mchezo huo kwenda katika hatua nyingine ya mikwaju ya penati ili kumpata mshindi wa mchezo huo.
Katika mikwaju hiyo ya penati The Might Elephant walipata penati 3 zilizofungwa na Ally Idd, Rashid Abdalah na Mwinyi Bwela huku Simon Minga akikosa penati yake kwa upande wa African Wanderers wao walipata penati moja tu iliyofungwa na Frank Nyambalapi huku Athanas, Michael Kalinga na Lisa Mwalipinda wakikosa penati zao.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika, mtandao huu ukazungumza na walimu wa timu zote mbili kwa kuanza na Bakari Makupe wa African Wanderers kwa kutaka kujua kipi kimesababisha kupoteza mchezo huo.
“Mchezo ulikua mzuri wachezaji wa pande zote mbili walijitahidi muda wote kwa kila hali lakini mpira ni dakika 90, dakia 90 zimemalizika lakini katika upande wa penati ni kama vile bahati, kunasiku unaweza kuamka salama hivyo kuna siku unaweza ukapiga vizuri au ukakosa”.
Pia mtandao huu ulimtafuta kocha wa The Might Elephant Francis Samata ili kujua amepokeaje matokeo hayo na kwanini timu yake imepoteza nafasi nyingi za kufunga.
“Mojawapo ni uwanja, wachezaji wangu wamejitahidi lakini mara nyingi walikuwa wanashindwa ku-control mpira vizuri, kitu kingine ni uzoefu lakini tunajitahidi kwasababu tupo ligi daraja la pili na tunawachezaji wengi wapya kwenye timu yetu”.