Leo vyombo vingi vya habari vya mjini Blida vimekua vikiuzungumzia mchezo kati ya Algeria dhidi ya Tanzania wa kuwania nafasi ya kupangwa kwenye hatua ya makundi kuwania kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi.
Yahaya Mohamed leo alipita kwenye mitaa ya mji wa Blida ambako ndipo mchezo kati ya Algeria dhidi ya Stars utapigwa na kukuta baadhi ya magazeti yakiwa yameandika habari zinazohusu mchezo huo, magazeti hayo yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kifaransa na Kiarabu lakini Yahaya aliongozana na mtanzania ambaye anasoma nchini Algeria kwa ajili ya kupata msaada wa lugha.
Matumaini ya wa-Algeria yamepelekwa kwa Yasin Brahimi pamoja na Sliman Islam ambaye alifunga magoli mawili kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam. Lakini pia hawakuacha kuandika kuhusu Samatta huku wakiisifia timu ya taifa ya Tanzania kuwa ni nzuri lakini wakiamini haiwezi kupata ushindi mbele ya timu yao kutokana na ubora wa wachezaji wanaounda kikosi cha timu hiyo.
Watu wengi mitaani wamekuwa wakizungumzia mchezo huo huku magari yakiwa yamefungwa bendera ya Algeria.
Katika pitapita, Yahaya akafanikiwa kukutana na kiajana mmoja aliyekuwa akimzungumzia Mbwana Samatta na kufanikiwa kufanya nae mahojiano ambapo alimuuliza kwamba anamfahamu vipi Samatta.
“Samatta ni mchezaji mkubwa, ni mchezaji wa Tanzania ni mzuri na timu ni nzuri, mechi itakuwa ni ngumu sana nyinyi mna Samatta, sisi tuna Sliman. Nampenda sana Sliman, Brahimi ni mchezaji ambaye anajua mbimu nyingi lakini mimi nampenda zaidi Sliman”, alisema kijana huyo.
Kiingilio cha mchezo huo kwa gharama ya kwaida ni dinari 300 ambayo ni sawa na shilingi 5000 au 6000 za kitanzania.
Bofya hapa chini kusikiliza story nzima wakati Yahaya alipokuwa kwenye mitaa mbalimbali ya mji wa Blida akijaribu kuangalia joto la mchezo kati ya Algeria dhidi ya Tanzania ambao utapigwa leo (Jumanne) saa 3:15 usiku kwa saa za Afrika mashariki.