Miongoni mwa matukio makubwa yaliyojitokeza kwenye mchezo kati ya Barcelona dhidi ya Vallencia ni weekend ya December 5, 2015 ni pamoja na shabiki wa Valencia kufariki dunia mara baada ya Santi Mina kufunga goli la kusawazisha dakika ya 86 kwa upande wa Vancia kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Mestalla.
Shabiki huyo wa Valencia alikuwa haamini kama timu yake ya Valencia ingeweza kusawazisha goli hilo baada ya Luis Suarez kuifungia Barcelona bao la kuongoza dakika ya 58, shabiki huyo alijikuta akishangilia kwa furaha iliyopitiliza goli la kusawazisha lililofungwa na Mina hadi kujikuta akipoteza maisha.
Mtandao huu umemtafuta daktari ili kutaka kujua hali hiyo husababishwa na nini kwasababu matukio yanayofanana na hilo japo sio ya vifo yamekua yakitokea hata kwa hapa Tanzania hasa zinapokutana timu za Simba na Yanga. Unaweza ukakuta timu inafunga goli la kusawazisha lakini shabiki wa timu husika anapoteza fahamu ikiwa timu yake ndiyo imefunga goli la kusawazisha.
Dr. Isack Maro ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo kwa kueleza kitaalamu hali hiyo husababishwa na nini.
Nimesikia kuhusiana na hii habari, ni habari kubwa dunia nzima, hili suala tusilipeleke kwenye furaha iliyopindukia na badala yake tuliweke kuwa ni mshtuko, unaweza kupata habari ya kufurahisha sana kwa ghafla au ukapata habari za kusikitisha kwa ghafla zote zitakushtua kwahiyo kilichotokea hapo ni lile tukio la ufungaji wa goli lilimfurahisha sana yule shabiki wa Valencia na matokeo yake akapata mshtuko.
Sasa moja ya sababu kubwa ambayo inaweza kutokea ambayo inaweza kuonekana ni moja ya tatizo, inawezekana alikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na matokeo yake ni kwamba kilichotokea ni changamoto kwenye mfumo wa damu.
Kadiri umri unavyokwenda na kama hatuli vizuri au tunakula vyakula vyenye mafuta kwa wingi ndiyo maana tunasema watu wafanye mazoezi kwasababu vyakula vyenye mafuta au wanga mara nyingi huwa vinahifadhiwa mwilini kama vimezidi na huhifadhiwa katika mfumo wa mafuta ikiwemo mafuta kama rehemu (cholesterol). Mafuta haya huhifadhiwa kwenye sehemu mbalimbali ikiwemo ndani ya mishipa ya damu.
Kadiri umri unavyokwenda, mafuta yanazidi kujazwa kwahiyo upenyo wa mishipa ya damu unazidi kupungua na baada ya muda kama likitokea tatizo lolote au changamoto yeyote, inawezekana hiyo mishipa ikaziba. Inapoziba ndiyo unapata kitu kama kilichotokea kwa huyo shabiki (Heart-Attack) lakini pia inawezekana ukapata kiharusi (strock) inategemea na mishipa ipi ambayo imepata changamoto.
Sasa kwa huyu kinachoonekana ni kwamba, labda yeye alikuwa na matatizo (sina uhakika) lakini kulikuwa na changamoto kwenye mfumo wake wa damu inawezekana alikuwa na shinikizo la juu la damu au alikuwa na tatizo la kuwa na rehemu kwa wingi vyote hivyo vinawezekana vilikuwepo. Sasa lile tatizo lilipotokea, akapata shock au mshtuko kwa hali ya kawaida ukipata mshtuko kitu cha kwanza kinachotokea ni kwamba kuna homorne inaitwa adrenaline ambayo humsababisha mtu aweze kupigana au kukimbia kwa nguvu.
Kwahiyo alivyoshtuka adrenaline ilimwagika, moja ya kazi ya adrenaline ni kushurutisha moyo ufanye kazi ya kusukuma damu kwa nguvu ili kumuwesha mtu kupigana au kukimbia pale anapokutana na tatizo kwa ghafla.
Kilichotokea kwa huyu shabiki ni kwamba baada ya adrenaline kumwagika na kushurutisha moyo usukume damu kwa nguvu, moyo ukasukuma damu kwa nguvu changamoto inayotokea kama mtu anamafuta kwenye mishipa yake ya damu na ghafla shinikizo la damu likapanda kitu kinachoweza kutokea kwasababu damu inapita kwa nguvu inabomoa mafuta yaliyojishikiza kwenye mishipa ya damu na kusafiri nayo.
Kwasababu inakuwa imeyabeba kama ‘bonge’, bonge hilo la mafuta likifika kwenye mshipa mdogo wa damu inamaana litashindwa kupita na maana yake litaziba njia. Na likiziba njia inamaana sehemu ambayo damu ilitakiwa iende haitofika kwahiyo changamoto zitaanza kuonekana za kutokufika kwa damu kwenye chembe hai.
Damu itashindwa kufika kwenye ubongo na matokeo yake ni kuona mtu anapata kiharusi lakini kwa bahati mbaya moyo ambao ni pump ya kusukuma damu lakini unajipelekea wenyewe damu kuhakikisha kwamba chembe hai ambazo zinaunda misuli ya moyo nazo zinapata hewa safi na kupata chakula.
Bahati mbaya moyo unamishipa midogomidogo sana kwahiyo kama kuna mabonge ya mafuta kwenye ile mishipa na shinikizo la damu likapanda ghafla na wakati huo bonge la mafuta likaziba njia na damu kushindwa kufika kwenye maeneo mengine kwahiyo chembe za moyo zikafa na kushindwa kufanya kazi kama ilivyotakiwa kufanya ya kuufanya moyo ujikunje na kujikunjua na kusukuma damu. Kilichotokea ni moyo kushindwa kufanya kazi ukawa umepata mshtuko, kwahiyo hiki ndiyo inawezekana kilichotokea, alieleza Dr. Maro.
Hii hapa sauti ya Dr. Isack Maro kama vipi click hapo chini umsikilize mwenyewe akifafanua kitu ambacho huenda kilimkuta shabiki wa Valencia aliyepoteza maisha baada timu yake kusawazisha goli wakati ikicheza dhidi ya Barcelona.