Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

BAO LA KAMUSOKO LILIUMALIZA ‘UCHAWI’ WA SPORTS? USHIRIKINA NI IMANI MBAYA TU…..

$
0
0
Kiungo wa Yanga Thabani Kamusoko akishangilia bao alilofunga dhidi ya African Sports
Kiungo wa Yanga Thabani Kamusoko akishangilia bao alilofunga dhidi ya African Sports

Na Baraka Mbolembole

Yanga SC walicheza kwa kiwango cha juu kwa dakika 3 au 4 tu za mwisho katika pambano waliloshinda kwa ushindi ‘mgumu’ wa 1-0 ugenini Mkwakwani Stadium, Tanga dhidi ya wenyeji na ‘vibonde’ wa ligi kuu African Sports.

Goli pekee la Thaban Kamusoko lilipatikana baada ya kila mchezaji aliyepasiwa mpira kuulinda, kuhakikisha unapitishwa katika njia sahihi huku ukifika kwa mlengwa. Mlinzi wa kushoto Mwinyi Hajji alipanda na mpira kwa umakini kisha, Geofrey Mwashuiya, Donald Ngoma + Kamusoko ambaye alimalizia pasi maridadi ya kichwa kutoka kwa Ngoma.

Nilipendezwa na namna Yanga walivyopanga shambulizi lao la mwisho katika mechi ila sikupendezwa  na namna klabu hiyo kubwa nchini ilivyoamini ‘kuhusu ushirikina’ kiasi cha kukataa kuingia katika vyumbavya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko.

Imezoeleka hivi sasa baadhi ya timu–hasa klabu kubwa, kugomea kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo kila zinapocheza Mkwakwani. Sababu kubwa ya ‘mgomo’ huwa ni ushirikina. Ni kweli TFF imekuwa ikitoa adhabu lakini bado vitendo hivyo havijakomeshwa, labda kwa kuwa adhabu yenyewe ni ndogo.

Yanga-Tanga 4

Ni wakati mwafaka wa kuzidisha adhabu kwa kitendo kama kilichofanywa jana na Sports na Yanga. Ili kuusafisha mchezo huu inapaswa sheria za mpira wa miguu kufuatwa na kama zinakiukwa mara kwa mara ni wazi kuwa kanuni hizo haziendani na ukubwa wa makosa.

Kimpira, hasa soka la kisasa imani ya ushirikina haipaswi kupewa kipaumbele. Ni kuutukanisha mchezo wenyewe, klabu, wahusika na wachezaji ambao sasa mechi nyingi huwa ‘Live’ zikionyeshwa na vituo vya matangazo ya televisheni.

Kila kitu huwa wazi na siamini kama Sports walitumia ‘uchawi’ ili kuidhibiti Yanga lakini kwa kuwa imani hiyo imezoeleka kwa timu za Tanga, Yanga waliamini hawawezi kushinda ikiwa wataingia katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa kuhisi tayari vimefanyiwa ‘uchawi’.

Timu ambayo imesajili wachezaji wa kulipwa, ikifanya mazoezi ya kukidhi mahitaji ya ligi kuu kama Yanga inashangaza sana kuona wakiamini katika ‘ushirikina’. Yanga ilicheza vibaya licha ya kuwa na uwezo wa juu zaidi ya Sports ambao hawakucheza kwa mipango ya kusaka ushindi.

Inawezekana baada ya suluhu-tasa dhidi ya JKT Mgambo Jumamosi ya wiki iliyopita (Mkwakwai) Yanga walijenga hofu ya ‘kurogwa’ kuliko kukubali ukweli kwamba walicheza vibaya. Hali ya timu hiyo imeshuka.

Yanga-Tanga 3

Nafikiri kwa sababu ya mapumziko matefu ya ligi, ila kwa namna walivyojipanga kukabiliana na ushirikina katika game ya jana dhidi ya Sports iliwafanya wacheze vibaya zaidi mbele ya timu ambayo haijapata ushindi katika mechi 10 mfululizo.

‘Ushirikina ni imani’ tena imani mbaya. Yanga hawapaswi kuamini hivyo kwa kuwa hali hiyo huwapunguzia wachezaji hali, uwezo wao wa kiuchezaji kwa kuamini kuwa chochote watakachofanya hawatafanikiwa kwa kuwa tayari ‘wamedhibitiwa-kiushirikina’.

Sivyo, ushirikina ni imani mbaya tu,  si sahihi hata kidogo na bahati mbaya Hans Van Der Pluijm na msaidizi wake walikubaliana na ukweli wa ‘kurogwa’ kiasi cha kukubali timu yao kupumzika mahala ambapo si tulivu, hasa ukizingatia wachezaji walikuwa wamepambana kwa dakika 45’ ngumu. mzungu naye kaamini kuhusu ushirikina kwenye soka!

Ni imani tu, ila ukweli kama Yanga wangecheza kwa umakini, mipango na kupiga mpira golini mara kwa mara kama alivyofanya Kamusoko dakika ya mwisho ya mchezo wangeshinda ushindi mkubwa zaidi. Bahati wamepata alama 3 muhimu, lengo lilitimia, ila walichemsha hasa kama klabu kubwa kugomea kungia katika vyumba vya uwanja kwa sababu za kishirikina.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>