Mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Tanzania Prisons utakuwa ni mchezo pekee utakaopigwa kwenye jiji la Dar es Salaam ambapo uwanja wa Azam Complex utakuwa kwenye patashika pindi vidume hivyo vitakapokutana leo jioni kwenye moja ya mechi za ufunguzi wa ligi kuu Tanzania bara (VPL) msimu huu.
Hii inatokana na matokeo yaliyopita katika miaka miwili mfululizo ambapo Tanzania Prisons imeibuka kuwa moja ya timu zinazoipa wakati mgumu timu ya Azam FC kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex uliopo kwenye eneo la Chamazi.
Prisons kwa misimu wiwili mfululizo haijafungwa na Azam FC kwenye uwanja wa Azam Complex hali iliyoamsha mihemuko ya wachezaji wa pande zote mbili. Leo jioni timu hizi zenye uzoefu na ligi kuu zitakwaana kwenye mechi ya ufunguzi VPL.
Mtendaji mkuu wa Azam FC Saad Kawemba amesema taratibu zote za maandalizi ikiwemo kupata vibali vya wachezaji wote wa ndani nan je ya nchi vimekamilika kwa asilimia mia moja, kilichobaki ni ni timu hizo kuoneshana kazi uwanjani.
Mlinzi wa kati wa Azam FC Aggrey Morris pamoja na nahodha msaidizi Salum Abubakar ‘Sure-boy’kwa pamoja wamesema, wapo tayari kwa pambano dhidi ya Prisons huku wakitamba kujiandaa vyema kuelekea mtanange huo na kuahidi ushindi kwenye mchezo huo.
Kwa upande wake kocha mkuu wa Azam FC Stewart Hall amesema “maandalizi yetu yalichukua muda mrefu na mechi nyingi, sasa ni wakati wa kuonesha kwa vitendo uwanjani. Uongozi umetupa kila tulichohitaji. Sasa ni wakati wetu kulipa kwa kucheza kwa bidii na kushinda kila mechi”.
Azam FC itafungua dimba kwa kucheza na Tanzania Prisons leo kisha itasafiri kwenda Shinyanga kuvaana na Stand United na baadae Mwadui FC siku ya Jumatano na Jumapili ijayo.