Juzi Alex Lwambano aliuliza kuhusu usajili wa Singida.
Je wale wachezaji walisajiliwa kwa mbinu za mwalimu yupi? Jibu inaonekana ni kama Wanasema Hans ndiye aliyeandaa mipango hiyo tayari.
Vipi Hemed Morocco kocha mpya alishirikishwa katika sajili hizo? Mimi sijui.
Ina wezekana kabisa mchezaji kusajiliwa bila ruhusa au maelekezo ya mwalimu. Si Unakumbuka Usajili wa Ander Herrera? Yule alishasajiliwa kipindi cha Fergie.
![]()
Ni kweli kila timu ina mipango yake na namna ya kufanya usajili. Sio kwamba kila mchezaji lazima asajiliwe na mwalimu. Ingekuwa hivyo basi makocha wangekuwa na timu zao kila saa wakisajiliwa wanaenda nazo.
Kuna malengo ya kibiashara ya timu kwa mfano usajili wa Fernando Torres, Usajili wa Gareth Bale. Inawezekana kweli Makocha wetu wa bongo hawana nguvu, lakini pia hata huko ulaya kuna wakati waalimu sio waamuzi wa mwisho wa usajili.
![]()
Tofauti yetu sisi na wale wa ulaya ni ipi?
Kwanza, nakubaliana na Yahya Njenge. Njenge anasema hivi, “ni vyema mchezaji au tuseme ni lazima mchezaji asajiliwe na falsafa za mwalimu. Mwalimu anapaswa kushirikishwa usajili wa mchezaji kabla ya yote”
(Bila shaka tuamini kuwa Hemed Morocco alipigiwa simu na akakubali sajili zote kwa mujibu wa Njenge).
Lakini Issa Maeda ana wazo tofauti.
Issa Ametoa sababu kubwa mbili za usajili hapa bongo kisha Lwambano akaongeza Moja.
![]()
Sababu ya 3 ya Issa ni kwamba, Usajili wa Tanzania ni wa roho mbaya wivu au kuzuia riziki za wengine.
Nilipomsikia Issa, nikakumbuka Sakata la Mzaliwa wa Kakole Shinyanga mdogo wangu Adam Salamba. Salamba ni rafiki yangu sana. Hivi majuzi niliongea nae kuhusu sakata lake la uhamisho kwenda Yanga. Hakunipa jibu la moja kwa moja lakini alikubali kwamba Yanga inamhitaji. Leo hii Salamba anatarajia kuvaa jezi nyekundu msimu ujao.
Hapo hapo nimekumbuka lile sakata la John Obi Mikel kwenda Man United kisha kuibiwa na Jose Mourinho.
![]()
Lakini Lwambano akauliza je wivu huu una faida kwa nani?
Njenge akajibu akasema mchezaji anapaswa kuangalia kama kuna uwezekano wa kucheza hiyo nafasi. Swali likaibuka kati yao, Je Salamba alihitajika Simba?
Binafsi kwa kuwa mimi nimjuaji nikajisemea moyoni kwamba wanataka kutengeneza kikosi kipana.
Hakuna kitu kibaya duniani kama kuiga usichokiweza.
Nani kawaambia kwamba mafanikio ya timu ni kuwa na kikosi kipana? Kikosi kipana ni kusajili ovyo bila mipango? Mbona timu kubwa kama Barcelona hawana huo mfumo wa kusajili wachezaji hovyo kwa ajili ya kupanua kikosi?
Mwisho wa siku Issa akatoa la moyoni
“kuna kijana mmoja bwana mdogo alinifuata akaniuliza, kaka, timu fulani wamekuja je niwakubalie? Nikamuuliza wametoa hela nzuri? Akaniji ndiyo kaka”
Kabla Issa hajamaliza kusimulia Lwambano akadakia na kusema
“wadogo Zangu maisha ndiyo haya haya, hizi ndoto za ulaya ni hadhithi za juma na uledi, maisha yenyewe magumu haya, pigeni hizo hela wakija na Milion 40 zao usikatae pigeni helaaa”
![]()
Issa akapigilia msumari kwa kudai kuwa hawa wachezaji wakihitajika Simba na Yanga wasikatae kabisa. Sasa hapa ndipo akili yangu ikakaa sawa. Kumbe lengo hapa sio timu ni hela/fursa.
Issa anasema
“Hakuna mchezaji wa kitanzania mwenye ufanisi wa muda mrefu. Mwaka huu atakuwa na msimu bora mwaka mwingine anapoteana hivyo linapokuja suala la Simba na Yanga ni Fursa ukiringa kwa lengo la kutaka kuendelea kuichezea klabu yako soka litaisha utakaribishwa mtaani na umasikini”
Katika sababu hii ya Issa ndipo sababu yake ya pili kuhusiana na usajili wa bongo ikaibuka.
Timu nyingi zinafanya usajili kwa sababu tu huyo mchezaji anatajwatajwa.
Kidogo hapa tunapaswa kukuna kichwa kabla hatujakubaliana nae
Nimekiangalia kikosi cha Yanga. Kuna wachezaji wengi binafsi yangu hawakupaswa kucheza klabu ile. Wengi wao walisajiliwa kwa sababu walitajwa tajwa sana. Na wengine walisajiliwa kwa sababu ile ile ya awali ya wivu (Buswita). Kuna wachezaji wanaonunuliwa bila timu kuangalia kama wanamhitaji au lah. Kwa mfano Simba ina mchezaji kama Said Ndemla, Ina Mzamiru Yasin ina Mo Ibrahim hawa wote wanachoma mahindi sasa jiulize Niyonzima alisajiliwa wa nini?
Leo hii Marcel baada ya kung’aa msimu paaap kavalishwa jezi nyekundu. Mo Rashid nae kaambiwa chagua moja, uendelee kula ndizi Mbeya au uje unywe juisi za Mo. Akasema usintanie maisha ndiyo haya haya.
Tena Mo anakwambia Okwi na Bocco hawamwambii kitu wajiandae kisaikolojia tu kukaa benchi. Unacheza na maisha mazuri nini?
![]()
Sababu ya mwisho ilikuwa ya Lwambano akasema “mchezaji kweli ana uwezo lakini wahusika wanatumia kigezo cha yeye kuwa na njaa kama sehemu ya kumpata bila kuangalia je atacheza wapi kivipi na kwanini”.
Issa Maeda akamtaja Jamal Mwambeleko ambaye alitokea Mbao Fc na kujiunga Simba, kama kielelezo cha wachezaji wazuri wanaozea benchi. Jamal anakumbana na na ushindani mkubwa sana kutoka kwa Erasto Nyoni, Tshabalala pamoja na Asante Kwasi.
Katika sababu hizi hakuna hata moja inayokwenda sawa na mawazo ya Njenge kwamba kocha anapaswa kushirikishwa kuhusiana na usajili wa mchezaji. Tena katika fukuafukua yangu nimekumbana na Fununu kwamba Omog aliondoka Simba kwa kuwa alikuwa analazimishwa wachezaji fulani wacheze au fulani asajiliwe.
![]()
Nimewaza sana sasa anayehusika na usajili ni nani?
Juzi juzi katika pita pita zangu nikakutana na kibonzo. Ulaya ukienda kuomba kazi unaombwa cheti, ujuzi wako na ueleze mipango yako, Lakini ukiingia Tanzania kuomba kazi unaulizwa hapa umeagizwa na nani? Kwa hiyo hata kwenye soka letu kuna uwezekano mkubwa usajili unafanywa maajumbani na sio maofisini.
Hatuna maskauti hatuna mawakawala hatuna wathaminishaji wa ufanisi wa mchezaji ila tuna namba za simu. Inapigwa tu oyaa dogo eeeh njoo Leaders Club hapa bosi anataka kuongea na wewe.
![]()
Inapigwa tu oyaa dogo eeeh njoo Leaders Club hapa bosi anataka kuongea na wewe.Makala hii imeandaliwa na Privaldinho (Instagram)