Liverpool wanataka kumsajili mshambuliaji wa Shakhtar Donetsk Alex Teixeira mwenye asili ya kibrazil na kama dili hilo litafanikiwa huo utakuwa ni usajili mkubwa wa kwanza kufanywa na kocha Jurgen Klopp tangu awe manager wa kikosi cha Liverpool.
Wekundu hao wako tayari kulipa kiasi cha pauni milioni 24.5 kwa ajili ya kuinasa saini ya nyota huyo mwenye miaka 26. Klabu ya nyota huyo ambaye pia anahusishwa na Chelsea imeweka dau la pauni milioni 39 kwa klabu inayotaka kumsajili mshambuliaji wao.
Klopp anataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kuwa washambuliaji wake wengi ni majeruhi kwa sasa, Danny Ings, Divock Origi pamoja na Daniel Sturridge wote wanauguza majeraha.
Usajili wa pauni milioni 32.5 kumnasa Christian Benteke umeshindwa kuzaa matunda yaliyotarajiwa baada ya timu hiyo kujikuta ikufunga mabao 25 katika mechi 22 za ligi kuu England hadi sasa.
Teixeira ameshatupia kambani jumla ya magoli 22 kwenye mechi 15 za ligi na magoli mengine 10 kwenye michuano ya klabu bingwa msimu huu.
Nyota huyo alianzia soka lake kwenye klabu ya Vasco da Gama ya Brazil kabla ya kuhamia Shakhtar mwaka 2010.
Klopp amemsajili kwa mkopo beki Steven Caulker wa QPR na amekamilisha dili la kinda mwenye miaka 19 Marko Grujic kwa pauni milioni 5.1 ambaye ameachwa kwa mkopo kwenye klabu ya Belgrade hadi majira ya joto.
Usajili wa Teixeira utakuwa ni usajili wa kwanza mkubwa kwa Klopp kwenye soko la usajili na mshambuliaji huyo atakuwa ni mbrazil wa nne kwenye kikosi cha Liverpool akiwa ametanguliwa na Lucas Leiva, Roberto Firmino na Philippe Coutinho.