Baada ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya Tanzania Prisons kumalizika, mtandao huu ulimtafuta nahodha wa’ wajelajela’ Prisons ya Mbeya Laurian Mpalile na kufanya nae maojiano ili kujua mambo kadhaa kuhusu kikosi cha maafande hao wa Magereza ambao wameshachapwa kwenye michezo yao miwili waliyocheza jijini Dar es Salaam wakwanza ukiwa ni ule waliopoteza kwa goli 2-1 mbele ya Azam FC.
Shaffihdauda.com: Dakika 20 za kwanza mlionekana kucheza kwa kuzuia zaidi uku mkitumia nguvu na mara kadhaa mlicheza sana rafu, kwanini mlianza kwa stahili hii?
Laurian Mpalile: Sisi tulikuwa tunacheza kama mwalimu alivyotuelekeza na siyo kama tulikuwa tunazuia, dakika za mwanzo tulikuwa tunawaangalia kwanza Yanga wanafanya mashambulizi yao kupitia wapi. Ndio maana dakika za kwanza hatukuwa tunashambulia sana.
Shaffihdauda.com: Japo mlicheza kwa nguvu na kuzui sana lakini ndani ya kipindi cha kwanza tayari mlikuwa mmeruhusu goli mbili, tatizo lilikuwa nini?
Laurian Mpalile: Hata goli mbili za kwanza tulizofungwa utaona zilikuwa ni kutokana na makosa ya golikipa, lakini sisi tunaheshimu hilo kwasababu ni makosa ya mchezo ambayo hata mchezaji mwingine anaweza kufanya.
Shaffihdauda.com: Mmepoteza mchezo wa pili mfululizo, mnakutana na Mbeya City ambayo imeshinda mechi moja na wote mtakuwa kwenye uwanja wa Sokoine, unautazamaje mchezo huo?
Laurian Mpalile: Mchezo dhdi ya Mbeya City utakuwa mgumu, sisi tunawaheshimu Mbeya City kwasababu ni timu nzuri, timu kubwa na inafundishwa na mwalimu mzuri. Uzuri wa Mbeya City hautufanyi sisi kuogopa kucheza nao.
Shaffihdauda.com: Mara nyingi mnapokutana na Mbeya City huwa wanawasumbua na mmekuwa mkipoteza mara nyingi mbele yao tutarajie nini, mtapoteza mchezo wa tatu mfululizo?
Laurian Mpalile: Hatuwezi kukubali kupoteza mchezo wa tatu mfululizo. Kwanza tutakuwa tunacheza mchezo wetu wa tatu na wakwanza tukiwa nyumbani, wao wameshacheza mechi mbili nyumbani na sisi tutautumia vizuri uwanja wa nyumbani ili kuibuka na ushindi.
Shaffihdauda.com: Kadi nyekundu aliyopewa mchezaji wenu Josephat, unadhani mwamuzi alikuwa sahihi kumtoa mchezaji wenu na nyinyi kubaki pungufu?
Laurian Mpalile: Kadi nyekundu ilikuwa ni maamuzi sahihi ya mwamuzi, kwasababu Josephat alikuwa ni mchezaji wa mwisho na alimfanyia Msuva ‘tackling from behind’ na ukifanya hivyo ndani ya boksi moja kwa moja inakuwa penati na kadi nyekundu.
Shaffihdauda.com: Ndani ya miezi sita timu yenu imebadili mackocha zaidi ya watau, unadhani hili linachangia nyinyi kufanya vibaya?
Laurian Mpalile: Kubadilisha makocha wengi kwenye timu nayo inachangia timu yetu kufanya vibaya kwasababu kila kocha anakuja na philosophy zake kwahiyo inakuwa vigumu kubadilika harakaharaka kuendana na matakwa ya kocha.