
Azam Media LTD na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF wamesaini mkataba wenye thamani ya shilingi bilion 2 wa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi za ligi kuu ya vilabu vya wanawake Tanzania (Tanzania Women Premier Legue) na ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (U-20).
Mkataba huo ni wa miaka mitano ambapo ligi kuu ya vilabu vya wanawake itaanza kwa kushirikisha vilabu 10 na ligi ya U20 itashirikisha vilabu vyote vinavyoshiki ligi kuu.
Kila klabu ya ligi kuu itawajibika kuwa na timu ya U20 kama kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa mashindano hayo ambazo zitatungwa na TFF na ligi hizo zitaanza msimu wa 2016-17.
Azam Media LTD imekuwa ikishirikiana na TFF katika kukuza na kuboresha tasnia ya mchezo wa mpira wa miguu nchini Tanzania kwa kuingia mikataba kama hiyo ya urushaji wa matangazo wa moja kwa moja katika ligi kuu Tanzania bara ijulikanayo kama Vodacom Premier League na mashindano ya Azam Federation Cup ambapo mashindano hayo yote yamemalizika msimu huu.
Licha ya hivyo, Azam Media imekuwa ikidhamini pamoja na kununua haki za matangazo ya ligi za mpira nje ya nchi kama Uganda (AUPL), Rwanda (ARF) na Kenya, ikiwa na dhumuni la kuendeleza na kuoresha kiwango cha soka katika ukanda wa Afrika Mashariki.