Na Ayoub Hinjo
Yuko wapi yule aliyesema imani inaponya? Katika hili hakukosea kabisa maana imani ya wanachama wa Yanga imemrejesha tena Manji. Imani ya matokeo ya uwanjani imemrejesha tena. Na katika yote imani ya harufu ya pesa imemrejesha tena. Imani inaponya inabidi tu tuamini katika hili.
Pongezi kwa Yusufu Manji kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa timu ya Yanga kwa mara ya pili mfululizo. Nadhani hakuna wasiwasi tena wa kukanyaga kinyesi kama umevaa viatu vya kuazima maana hufanya watu kutembea kwa wasiwasi na taratibu kuhofia kuviharibu.
Manji amerudi tena pale mitaa ya Jangwani lakini sasa sijui amerudi na nini maana kila alichofanya katika utawala wake uliopita kilionekana kwenda vizuri bila shida yoyote kwa sababu ya uwepo wa pesa. Nadhani kurejea kwake ni muendelezo wa pale alipoishia. Katika muendelezo huu inawezekana Manji akafikiria kuhusu timu ya vijana na uwanja ule wa Kaunda.
Unadhani amerejea kwa bahati!? Hapana amerejea tena sababu ndiye mtu sahihi aliyefanikiwa kukidhi haja za mashabiki na wanachama wa Yanga ndani ya uwanja. Mambo yaliyo nje ya uwanja yanakuwa mazuri kwa shinikizo la mambo mazuri pia yanayotokea ndani ya uwanja, hivyo ndivyo ilivyo. Manji amewekeza kwenye kikosi ili kuzima mambo ya nje ya uwanja ambayo yanaitesa Simba kwa sasa kutokana na kushindwa kusimama imara ndani ya uwanja.
Manji amerejea tena huku akiwa ametimiza, ahadi ya kuidhoofisha Simba ndani ya uwanja. Yanga wameonekana imara zaidi ya watani wao Simba kwa miaka ya karibuni hasa ndani ya uwanja ambako ndiyo wanachama wengi hupima uzuri na mabaya ya viongozi. Sidhani kama Aveva angekuwa akisumbuliwa na kelele za wanachama kama Simba wangekuwa wanapata matokeo chanya ndani ya uwanja.
Nadhani hata wapinzani waliokuwa wanataka kushindana na Manji katika kuwania uongozi waliamua kukaa kando sababu hali ya timu yao inajulikana hasa kipindi hiki ambacho wanashiriki michuano ya kimataifa. Asingekuwa Manji nani angelipa gharama za ndege!? Nani angelipa mishahara ya wachezaji bila kukopwa kwa muda sahihi!? Nani angelipa malazi ya timu kwenye hoteli!? Na mambo mengine mengi maana kila kinachofanywa sasa na Yanga kinahitaji pesa.
Hakuna kingine wanahitaji zaidi ya kushinda makombe tumeshuhudia Yanga wameshinda makombe mawili ya ndani,ligi kuu na kombe la FA chini ya utawala wa Manji. Labda ni nini wanahitaji zaidi ya kufika mbali katika kombe la shirikisho? Hakuna wa kuwapeleka mbali zaidi ya Manji ambaye anawekeza kwenye timu katika kuleta wachezaji bora na kuwalipa mishahara vizuri.
Mpinzani mkubwa wa mafanikio ya Yanga miaka ya karibuni ni Azam. Kwa misimu minne wamekuwa wanakimbizana na kubadilishana nafasi mbili za juu sasa kwanini wanachama wasimpe timu tena Manji? Maana huwa wanasema dawa ya moto ni moto. Katika hili nawaunga mkono. Ubora wa kikosi cha Yanga upo katika mikono ya Manji ambaye anatimiza kila kitu kwa timu kama ilivyo kwa wapinzani wake Azam labda atawekeza zaidi na zaidi atakapoona Simba imesimama tena na wanatembea bila kuchechemea.
Manji amerejea tena. Amerejea kutokana na matokeo chanya ya ndani ya uwanja,tusingemuona tena amerejea katika kiti chake endapo timu ingekuwa hovyo bila kupata matokeo.