Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

WARAKA WANGU KWA TFF: “NI TFF PEKEE INAWEZA KULIFANYA SOKA LETU LIWE BORA KAMA LINAVYOPASWA KUWA”

$
0
0

Jengo-la-TFF1

Na Alcheraus Mushumbwa

TFF – ni kifupi cha ‘Tanzania Football Federation’ kwa kimombo, yaani ‘Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania’ kwa Kiswahili lugha yetu adhimu. Ni shirikisho au taasisi ambayo ndio yenye dhamana ya kuratibu shughuli zote zinazohusu mchezo huu hapa nchini; ndio wanaoendesha na kusimamia mambo yote yanayohusu soka la nchi yetu.

Kwahiyo, TFF ndiye baba na ndiye mama wa soka hapa Tanzania. Kwa majukumu haya, matokeo yoyote yale kuhusu mpira wetu wa miguu ni TFF ambao wanapongezwa au kulaumiwa kwa asilimia kubwa. Kwahiyo ni jukumu la shirikisho hili kuhakikisha soka letu linakuwa na mafanikio zaidi kuliko matatizo!

Pamoja na ukweli usiopingika kuwa suala la michezo (soka) ni jukumu la jumuiya nzima ya watanzania na si TFF pekee, kwa mfano: wananchi wote, serikali na TFF. Bado, ili kufanikisha kilele cha mafanikio ya hali ya juu ambacho watanzania wengi tuanataraji kukiona TFF hawana budi kuwa mstari wa mbele. Ni wazi na inaeleweka takribani kwa umma wa wapenda soka wengi na hata wale wasiofatilia soka kuwa mpira wetu wa miguu umekuwa na matatizo mengi kuliko mafanikio.

Hili si suala linalopendeza kwa nchi yetu na kwa wapenda soka kwa ujumla. Je, sisi ndio hatutaki kufanikiwa katika soka kama Brazil, Hispainia, Ujerumani au Ghana, Ivory Coast, Nigeria n.k? Jibu ni kwamba TUNATAKA! Je, kama tunataka kufanikiwa, tunafanya nini au mikakati gani? Majibu yanaweza kuwa mengi na ya kujenga ilimradi tuweze kufanikiwa. Na mimi ninayo mawazo yangu juu ya hili na ndilo lengo la waraka huu kwa TFF.

Moja, kwa kuwa TFF kama taasisi ina wataalam ambao wanaweza kukaa na kuandika pendekezo zuri la mikakati ya namna ya kuinua kiwango cha soka na kuipelekea serikali pamoja na wadau wengine ukaanzishwa mpango maalum wa kuzungukia nchi nzima kushawishi na kutoa elimu juu ya faida za jamii kuwekeza katika michezo hasa soka ili elimu hii iwajae watanzania pamoja na walezi na wazazi kuwa michezo hasa mpira wa miguu ni sehemu ya maisha na ajira kwa vijana na kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Huu unakuwa kama mpango wa haraka, lakini pia TFF iweze kuwa chachu ya ushawishi kwa serikali kuhimiza mchezo wa soka kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu kwa kuanzisha somo la michezo kwa wanafunzi ili wanafunzi hawa wanapohitimu tayari kuwemo wale ambao wamechagua soka kama fani yao.

Pia, TFF kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato pamoja na kuomba ruzuku serikalini ili kujenga shule za mchezo wa soka na vyuo angalau chuo kimoja kwa taifa pamoja na shule moja ya soka katika kila kanda ambazo zinakuwa zinasimamiwa na TFF. Sanjali na hili, bado TFF inao ushawishi mkubwa kuunga mkono na kushawishi wadau wa soka katika kuanzisha shule za soka nyinginezo.

TFF waanzishe mpango maalum wa kusaka vipaji vya soka mara moja kila mwaka katika kona zote za nchi hii kwa ngazi mbalimbali za miaka, kuanzia miaka 10, 12, 14, 17, 19, 20 na kuendelea. Hawa watakuwa wanasakwa kwa mchujo kulingana na vigezo vya kitaalamu vilivyowekwa na TFF, na wanaofuzu wanapelekwa kuendelezwa katika shule hizi za soka.

Wapo makocha na walimu wengi waliobobea katika taaluma ya mpira wa miguu ambao hawa ndio wanaopaswa kutumiwa kusaka vipaji ambavyo vinapaswa kupelekwa kuendelezwa katika vyuo na shule za soka kwa ajili ya kuwapata akina Ulimwengu na Samatta wengi.

Ili kuendeleza ukuaji wa vipaji vya mpira wa miguu kwa vijana wadogo, ni jukumu la TFF kuiomba serikali kibali cha kupeleka makocha wenye leseni wa madaraja ya juu na kati ili waende kutoa mafunzo kwa walimu huku shuleni, ambapo walimu hao ndio watakao kuwa wakufunzi wa michezo kwa wanafunzi wetu kwa kila shule na vyuo hapa nchini. Inaweza kuwa angalau walimu wawili kwa kila shule kuanzia msingi hadi chuo kikuu.

Tatu, mara baada ya TFF kuweza kubainisha vijana wenye vipaji vya soka na kuwapeleka katika shule na vyuo vya michezo, basi angalau kwa kila mwaka kunakuwa na ligi ya shirikisho la mpira wa miguu kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 na 19. Ligi hii iwasaidie vilabu vya soka hapa nchini kusaka vipaji na kuwasajili hawa vijana katika timu B zao na katika timu za wakubwa. Ili kupata soko la usajili kwa vijana hawa wanaopatikana katika ligi ya TFF, ni lazima sheria ya kuvilazimisha vilabu vyetu vya ligi kuu na ligi daraja la kwanza kuwasajili hawa vijana ianzishwe.

Hii itakuwa imesaidia kuhimarisha na kuifanya sheria ya TFF ya kuvitaka vilabu vya ligi kuu kuwa na timu B za umri chini ya miaka 20. Ambapo, vilabu vikishakuwa na timu hizo ni lazima TFF iandae mashindano ya ligi kwa timu B za vilabu. Hii itafanya mpira uchezwe kwa ngazi zote na kupata wachezaji wengi wa soka. Pia iwepo kanuni ya kuvitaka vilabu kila msimu vinapandisha angalau wachezaji 3 hadi 5 kutoka timu B zao na si chini ya wachezaji 3 wanatakiwa kuwa wanaanza katika kikosi cha kwanza cha timu ya wakubwa, ili kuwapa uzoefu wachezaji hao na kupata nafasi ya kucheza ili waweze kuwa hazina ya baadae.

Nne, ni lazima TFF ianzishe sheria ya kuvitaka vilabu vyetu vya mpira wa miguu kwa wanaume kuwa na timu za wanawake, kama zilivyo Ulaya (mfano: Arsenal ladies, Manchester United ladies n.k), ambapo hapa Tanzania na sisi tutakuwa na vilabu vya timu za wanawake kama Toto African ladies, Mtibwa Sugar ladies, Mwadui FC ladies n.k pamoja na timu za ligi daraja la kwanza kuwa na timu za wanawake. Kama ilivyo ligi ya soka kwa timu B za vilabu, pia iwepo ligi ya TFF kwa wanawake kwa vilabu husika.

Jambo hili hakika litafanya soka kwa wanawake lichezwe kwa kiwango cha hali ya juu na kupata wachezaji wengi timu ya taifa ya wanawake na watakaopata fursa za kucheza nje ya nchi katika ligi mbalimbali.

Tano, ili kuufanya mpira wa miguu Tanzania kuwa wa kiuweledi zaidi, wa kisasa na wenye ushindani hasa katika ligi, TFF watunge sheria na kanuni ili kuvifanya vilabu vitoke katika mfumo wa kishamba wa umiliki wa wanachama bila hisa na kuruhusu uwekezaji wa watu binafsi au umilikiwa wa wanachama au vikundi vya watu katika vilabu kwa hisa. Maana yake ni kwamba, ni lazima kila kilabu kiendeshwe kisasa, kibiashara ambapo wawekezaji wanaweza kununua sehemu ya umiliki wa timu au timu nzima kama ilivyo Azam FC. Isiruhusiwe timu yoyote kupewa usajili na kibali cha ligi kuu bila kuwa katika mfumo wa kibiashara yaani umiliki wa hisa.

Sheria hii itafanya vilabu vyetu kuendeshwa kisasa na kiutaalamu zaidi na itatoa mwanya kwa wadau wa soka kuwekeza katika vilabu kwa kuvinunua moja kwa moja au kuwa na sehemu ya umiliki. Uzuri wa jambo hili utaondoa ukiritimba wa baadhi ya watu kutaka kuzifanya timu ziwe mali yao, lakini pia wawekezaji hawatakubali kuona hasara wakati wamewekeza pesa nyingi katika vilabu hivyo.

Hakutakuwepo na masuala ya vilabu vidogo kulalamikia mapato, kulia na udhamini mdogo, ukata wa fedha za kuviendesha n.k. Mishahara na malipo ya wachezaji na uongozi kwa kila kilabu yatakuwa ni ya kuridhisha na njaanjaa za kurubuniwa na kupanga matokeo zitapungua pia. Uendeshaji wa vilabu wa namna hii, ujengewe kanuni ya kila kilabu kuwa na uwanja wake wa nyumbani na uwanja wa mazoezi kama ilivyo Ulaya. Jambo hili litaufanya mpira wetu uwe wa kitaalamu kivitendo kuliko kama ilivyo kinadharia.

Kimsingi, kama nilivyodokeza kuwa waraka huu ni maoni yangu jinsi ambavyo TFF kwa kushirikiana na wadau inaweza kuinua soka letu na kulifanya liwe soka bora la kiutaalamu kama ilivyo kwa nchi zilizofanikiwa kama za Ulaya na Amerika. Ni matumaini yangu kuwa endapo TFF watakaa na kusoma waraka huu na kujaribu kuyatafakari maoni yangu bila kuzingatia hadhi na uwezo wa mtoa maoni, wanaweza kupata angalu jambo la namna ya kukuza soka letu. Yangu ni hayo.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles