Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

CHUNGU, TAMU, MIEZI 32 YA MALINZI TFF – Part III

$
0
0

IMG_0287

Na Lasteck Alfred

ZIMEBAKI siku chini ya 98,  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, atimize miaka mitatu tangu aiingie madarakani usiku wa kuamkia Oktoba 28, 2013 kuliongoza shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini.

Kuna mambo mengi yanayohusu soka la Tanzania yaliyofanyika katika kipindi hiki cha miezi 32 na siku 27 cha uongozi wa Malinzi, lakini sehemu kubwa ya mipango na uamuzi uliofanya na utawala wa rais huyo haukuwa na tija kwa maendeleo ya mchezo huo nchini tena huenda ukawa hauambatani na sera za utawala bora.

Makala haya yanaangalia baadhi ya mambo mabaya na mazuri yaliyofanywa na uongozi wa Malinzi tangu aingie madarakani kumrithi mtangulizi wake, Leodegar Tenga. Swali kubwa ambalo mdau wa soka nchini anaweza kujiuliza ni je Utawala bora kwa Malinzi uko wapi?

TIKETI ZA KIELEKTRONIKI

Kutokana na maandalizi yasiyo mazuri, TFF tangu ilipotambulisha tiketi za kielektroniki walishindwa kuendesha mambo jambo ambalo liliifanya shirikisho hilo kusitisha lakini mapema mwaka huu waliagizwa kurudisha tiketi za kielektoriki lakini wakakaidi wakisema kuwa wataanza msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Kutokana na hilo TFF ilirudi kwenye mfumo wa kizamani wa TFF kuchapa tiketi bila hata kutoa zabuni. Mwaka jana Aprili, moja ya chombo cha habari kilimnukuu Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa aliliambia gazeti hilo kuwa walikuwa wakichapisha tiketi za kawaida, kazi inayotekelezwa na kampuni tofauti tofauti, kulingana na mahitaji ya mechi husika.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mtendaji huyo wa TFF alieleza kuwa wamelazimika kutumia utaratibu huo kwa kuwa hawawezi kuwa na kampuni ya kudumu ya kufanya kazi hiyo kutokana na mkataba wa CRDB kwa tiketi za elektroniki.

“Mfumo ule ulipoanza, kuna vitu vilionyesha upungufu, tulichokifanya, tulikaa na CRDB na kukubaliana, ila kuna vitu tulitaka viboreshwe, kazi hiyo inaendelea na watakapokuwa wamekamilisha, utaratibu wa kutumia tiketi za elektroniki utaendelea,” alisema.

KUKAIDI AGIZO LA WAZIRI MKUU

Mnamo Februari 18, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, alimuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuhakikisha tiketi za kielektroniki zinatumika kwenye mechi zote za soka zitakazochezwa kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo ili kupunguza ubadhirifu wa mapato ya milangoni ambao umekuwa ukijitokeza kila kukicha kutokana na matumizi ya tiketi za kawaida kutoa mianya ya fedha hizo kutumika vibaya.

“Tuna wataalamu wa kutosha hivyo zoezi la kutumia tiketi za elektroniki linatakiwa kuanza mara moja na ikiwezekana zoezi la mashabiki kununua tiketi kupitia simu zao liwe linaanza wiki moja kabla ya mechi,” alisema Majaliwa.

AVUNJA KAMATI ZOTE TFF

Katika hali ya kushtusha ambayo ilionekana kama alidhamiria kuuonyesha umma kwamba kamati zilizoundwa na Tenga zilikuwa na dosari, mara tu baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya urais wa shirikisho hilo, Malinzi alitangaza kuzivunja kamati zote za TFF na kuahidi kuziunda upya. Baadaye aliunda kamati na sekretarieti iliyozodolewa mno na wadau wakidai ilijikita katika kujuana na kujali zaidi watu wanaotoka mkoa wa Kagera.

ASAMEHE WAFUNGWA WOTE TFF

Uamuzi mwingine wa kushangaza ambayo Malinzi aliufanya mara tu baada ya kukabidhiwa kipaza sauti kwa ajili ya kutoa hotuba yake ya kwanza kama Rais wa TFF, ni kutoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa na TFF kutokana na makosa mbalimbali ya kimpira.

AMTIMUA ANGETILE KINYAMA

Kuondolewa kinyama kwa aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, ni moja ya ‘uamuzi mgumu’ uliofanywa na Malinzi mara tu baada ya kukabidhiwa rungu la kuliongoza shirikisho hilo.

Mara tu baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na Tenga Novemba 2, 2013, Malinzi aliitisha kikao cha kwanza cha kamati yake ya utendaji kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Baada ya ajenda kuu ya kikao, Malinzi aliwafukuza ukumbini watendaji wote wa kuajiriwa kisha akawaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa hakuwa na imani na katibu mkuu wa shirikisho (Angetile) na baadhi ya watendaji wengine wakiwamo Sunday Kayuni aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Saad Kawemba aliyekuwa mkurugenzi wa mashindano wa shirikisho.

Kulitokea mvutano baina ya wajumbe, lakini baadaye walikubaliana Angetile apewe likizo ya lazima iliyoambatana na malipo ya mishahara ya miezi miwili iliyokuwa imebaki katika mkataba wake na TFF.

Malinzi hakuishia hapo kwani alikwenda TFF akiwa na Angetile akamlazimisha akabidhi ofisi usiku wa manane kisha kumnyang’anya gari aina ya Toyota Rav4 alilokuwa alikitumia kama kiongozi wa TFF. Uamuzi huo uliwashangaza wengi, wakidai ulikuwa ni unyama kumlazimisha Angetile kukabidhi ofisi usiku mnene ilhali bendera ya taifa, bendera ya TFF, bendera ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na bendera ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zilikuwa zimeshashushwa kwenye ofisi za shirikisho hilo, pia kumwacha Angetile pale Karume akiwa hana usafiri wa kumpeleka nyumbani.

LASTECK ALFRED NI MWANDISHI NA MCHAMBUZI WA MICHEZO KWENYE GAZETI LA LETERAHA


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>