Ikiwa kama Paul Pogba atasajiliwa na Manchester United kwa ada ya uhaisho ambayo inatajwa kuvunja rekodi, basi itathibitisha rasmi utajiri uliopo kwenye ligi ya England. ligi ambayo ndio maarufu kuliko zote ulimwenguni. Ule utamu ama ladha ya kuitazama Ligi Kuu England pasi na shaka ni kubwa huku kwa upande wa haki za kurusha matangazo ya live ikizidi kuifanya kuwa ligi ghali zaidi duniani.
Licha ya matumizi makubwa ya pesa, na vipaji vya wachezaji wanaonunuliwa, kuna swali kubwa sana la kujiuliza juu ya tasnia ya soka nchini England.
Paul Pogba ni mfano hali wa jambo hilo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ni kiungo mwenye uwezo wa kudrive timu, kupeleka mashambulizi, mwenye mwili uliojengekea kuanzia miguuni mpaka juu bila ya kusahau nguvu alizonazo. Kuna kitu kimoja ambacho ana tatizo kubwa..anakosa ile kasi ama wepesi wa kuendana na kipute cha EPL.
Lakini Pogba pengine ni mchezaji ambaye anakosa ile thamani halisi ya paundi mil 100, ambayo inatajwa kuwa ndio price-tag yake. Kweli bado kijana mdogo, lakini anakosa vile vitu ambavyo Lionel Messi, Cristiano Ronaldo au Luis Suarez wanavyo. Vitu ambavyo vingekuwa ni mwiba mchungu kwa wachezaji wa Ligi ya England.
Misisitizo mkubwa kwnye ligi hii uko kwenye matumizi ya nguvu. Watendaji, sio wale wanaoangalia na kufikiri wanafanya ndio wanafanya hivyo. Kama mchezaji ni kijana halafu mwepesi, una kasi na mbio, basi ni rahisi kufiti kwenye mfumo. Pogba na umbo lake kubwa lililosheheni misuli ana kazi kubwa ya kufanya. Ubora wake katika kumiliki na kuudhibiti hauwezi kuwa na tija sana kwa Man United kama ambavyo ingekuwa kwa upande wa Barcelona au Real Madrid. Anahitaji kuwa mwepesi na mwenye kasi kubwa.
Uimara na matumizi makubwa ya nguvu ni sababu kubwa ya utofauti wa ligi hiyo na ligi nyingine. Hali hiyo pia inasababisha kwa kiasi kikubwa kutotabirika kwa matokeo miongoni mwa timu. Kasoro kubwa ya EPL ni kwamba wakati mwingine kunakosekana muunganiko mzuri wa timu. Hali ambayo inapelekea katika miaka ya hivi karibuni timu nyingi kutoka England kushindwa kufanya vyema kwenye Michuano ya Ulaya, tangu mara ya mwisho Chelsea alipochukua kombe hilo mwaka 2012.
Rafa Benitez ameshawahi kusema kwamba kwenye ligi ya England mbinu ni sehemu ndogo sana ya mchezo. “shindania mpira wa kwanza, mara ya pili fanikiwa kuupata,” Benitez alisema wakati akitoa maoni yake juu ya mikakati ya namna ya kupambana katika soka la England. Pengine inawezekana aliongeza chumvi lakini kuna chembechmbe za ukweli fulani ndani yake.
Sam Allardyce, bosi mpya wa England, ni moja ya watu wanaohusika kwa hili au waasisi wa soka la England la sasa. Wakati ule akiwa bosi Bolton Wanderers na makocha wengine waliokuwa kwenye ligi hiyo walikumbana na janga kubwa sana. Arsenal ambayo ilikuwa ikicheza soka la pasi nyingi na nafasi huku wakitumia nguvu kiasi na kasi kubwa walileta dhahma kubwa mno.
Akaamua kubadilisha mbinu. Alichokifanya baadaye ni kuhakikisha anapambana kupunguza kasi ya vijana hao wa Arsene Wenger. Akaanza kutumia mfumo unaotaka matumizi makubwa ya nguvu huku kasi ikihitajika kwa kiasi kikubwa. Katika mfumo huo, ujuzi mkubwa haukuwa jambo lenye umuhimu sana. Alienda tofauti kabisa na Arsene Wenger ambaye kwake mbinu nyingi na ujuzi mkubwa ndio vilikuwa kipaumbele kwake. Tangu hapo, taswira ya soka la England ibadilika kabisa na kuja mfumo mpya.
Mbaya zaidi ni huyo huyo Allardyce ambaye ni muasisi wa mfumo huo wa England kwa sasa, amepewa timu ya taifa baada ya kutofanya vyema kwenye Michuano ya Euro mwaka huu. Mfumo huu si aliyekuwa kocha wa timu hiyo Roy Hodgson wala wachezaji wake ambao wameweza kuendana nao vilivyo. Ni waumini wa kusukuma mpira mbele bila hata uelekeo maalum.
Soka la England limejaa fedha, mapambano makali na msisimko, lakini limekosa ile hali ya kuwafanya wachezaji kuwa na uwezo wa kufukiria mbinu mpya. Uwanjani, wachezaji wanakuwa na muda mchache sana wa kutafakari. Wanapokutana na vilabu bora ulimwenguni huwa wanapata shinda sana. Kama unakumbuka Liverpool waliitoa Borussia Dortmund kwenye Michuano ya Europa lakini wakaja kuadhibiwa vibaya na Sevilla kwenye mchezo wa fainali kutokana na Sevilla kucheza kwa mbinu na akili nyingi zaidi ya Liverpool.
Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich na Atletico Madrid wanaweza kupata matokeo bora endapo tu wao ndio wanakuwa wameudhibiti mchezo. Lakini kwa upande wa timu za England huwa zinaweza kufanya maajabu wakati wowote hata kama mchezo unakuwa hautabiriki kutokana na aina ya mchezo wanaocheza.
Pogba anaweza kuwa mtu sahihi kucheza kwenye ligi ya England, lakini endapo tu ataweza kubadilika na kuendana na aina ya soka la England. Kweli ni mtu ambaye ni vigumu kuchukua mpira miguuni mwake lakini anahitaji kufanya zaidi ya hapo ili thamani yake iendane na ubora wake.
Swali la kujiuliza la mwisho ni je, ataweza kuongeza msisimko na kuleta utofauti kwenye timu? Ataweza kurudisha furaha ya United ambayo imepotea kwa muda mrefu sasa na kuwafanya kuwa wawaniaji wa taji la Ligi ya Mabingwa badala ya kuwa washiriki kama siku hizi? Tusubiri.
Ikumbukwe tu haya yote yanakuja kwasababu ya kiasi kikubwa ambacho kinatajwa kuweza kutolewa ili kuinasa saini yake. Kwa maana hiyo basi, macho na masikio ya wapenzi wengi wa Manchester United yatakuwa yakielekezwa kwa Pogba kufanya maajabu kwenye timu hiyo.
Lakini mwisho wa yote ni kwamba, Pogba ni aina ya wachezaji ambao angeweza kucheza vizuri zaidi katika ligi ya Uhispani kutokana na aina ya soka analocheza, soka lenye ufundi mwingi na kadhalika.