Mshambuliaji mpya wa klabu ya Simba Leudit Mavugo amesema, anaamini klabu yake mpya itafanya vizuri katika msimu wa ligi kuu ya Tanzania bara ambao unatarajia kuanza hivi karibuni.
Mavugo ametoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki dhidi ya AFC Leopards ya Kenya katika kilele cha kuadhimisha Simba Day jana jioni kwenye uwanja wa taifa.
“Nawashukuru mashabiki wa Simba kwa jinsi walivyoni-support nawatakia kila laheri, tutaendelea kufanya vizuri huu ndio mwanzo,” Mavugo aliimbia shaffihdauda.co.tz muda mfupi baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Leopards.
“Simba ni timu nzuri sana nimefurahia namna viongozi, wachezaji na mashabiki walivyonipokea. Naamini msimu huu tutafanya vizuri.”
“Nimefurahi pia kufunga kwenye mechi ya kwanza, nimefurahi sana.”
Mavugo ambaye alifunga goli moja kati ya manne kwenye mchezo wa jana, alimtengenezea pia nafasi ya kufunga winga mpya wa klabu hiyo Shiza Kichuya aliyefunga bao la tatu.
Mrundi huyo aliyekuwa akiwindwa na Simba karibu kwa miaka miwili sasa, tayari ameshawavutia mashabiki wengi wa Simba walioushuhudia mchezo wa jana.