Paul Pogba amesema “ni muda muafaka kurudi Old Trafford” baada ya kukamilisha usajili uliovunja rekodi ya dunia wa paundi milioni 89 kutoka Juventus kwenda Manchester United.
Kiungo huyo mwenye miaka 23 amerejea Old Trafford baada ya kuwa nje kwa miaka minne tangu alipoondoka katika klabu hiyo kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni 1.5 mwaka 2012.
Pogba ambaye amesaini mkataba wa miaka 5, ameongeza kwa kusema kwamba: “Hii ni klabu sahihi kwangu kupata mafanikio yote ninayotarajia.”
Nyota huyo ambaye aliisaidia Ufaransa kufika fainali kwenye michuano ya Euro mwaka 2016 ameshinda mataji manne ya Serie A kwa miaka yote aliyocheza Juventus.
Ni mchezaji wa nne kusajiliwa na Mourinho ndani ya United baada ya beki wa Ivory Coast Eric Bailly, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Sweden Zlatan Ibrahimovic na mshambuliaji wa Armenia Henrikh Mkhitaryan.
Itakuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 kwa klabu ya England kulipa ada ya uhamisho uliovunja rekodi ya dunia tangu walipofanya hivyo kwa Alan Shearer kutoka Blackburn Rovers kwenda Newcastle United walipolipa paundi milioni 15.
Pogba alijiunga na United kwa mara ya kwanza akitokea klabu ya Le Havre ya Ufaransa mwaka 2009 akiwa na miaka 16 lakini hakupata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza kabla ya mkataba wake kumalika July 2012.
Ameichezea Juventus mechi 178 na kufunga magoli 34 kisha kuisaidia klabu hiyo kufika fainali ya Champions League mwaka 2015.
Pogba amesema amamayake alimwambia ipo siku angerejea tena Old Trafford na hapo ndipo hatima yake ilipo.
Akizungumza na MUTV amesema: “Nimerudi Carrington. Imekuwa kama nimerejea nyumbani. Nilikuwa kama nimekwenda likizo tu.”
Paul Pogba akifanya mahojiano kwa mara ya kwanza na Manchester United TV