Na Baraka Mbolembole
MSHAMBULIZI wa Mbeya City FC, Ditram Nchimbi anaamini kikosi chao kina ubora wa kutosha kuifunga Simba SC katika pambano la ligi kuu Tanzania Bara jioni ya leo. City itawavaa Simba katika uwanja wa Sokoine, Mbeya ikiwa nafasi ya nne na alama 12 baada ya kucheza game nane.
“Tulipoteza michezo yote miwili msimu uliopita, ndiyo mpira wa miguu ulivyo, ila imebidi ifike mwisho sasa, tumejipanga kupinga hilo,” anasema Ditram katika mahojiano niliyofanya naye mapema siku ya leo.
“Itakuwa mechi ngumu ila tuko vizuri na tumejiandaa vya kutosha. Niseme tu, Simba kazi wanayo japokuwa filimbi ya mwisho ndiyo itakayoamua nani mbabe,” anasema, Ditram ambaye amepiga pasi mbili za magoli na kufunga goli moja msimu huu.
“Itakuwa mechi yangu ya tatu vs Simba (Simba 6-1 Majimaji, Simba 2-0 City game za msimu uliopita) na zote hizo nilitumika kama mchezaji wa pembeni.”
“Nashukuru sasa mwalimu (Kinnah Phiri) ameniamini na kunichezesha kama mshambuliaji wa kati, nafasi ambayo naipenda na kuimudu vizuri,” anasema, Ditram ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi daraja la kwanza akiwa na kikosi cha Majimaji FC msimu wa 2014/15.
Akiwa na miaka 23 sasa huku akiwa ameshafanikiwa kufunga magoli matano katika ligi kuu, Ditram ambaye alijiunga na City wakati wa dirisha dogo msimu uliopita ameanza katika kikosi cha kwanza mara mbili msimu huu wakati timu hiyo ilipocheza na Mwadui FC na Stand United, huku game 6 akiingia kama mchezaji wa akiba.
“Nina furaha kuanza katika kikosi cha kwanza katika michezo miwili iliyopita baada ya kutumika kama mchezaji wa akiba katika game 6 za mwanzo. Nimewaona mabeki wa Simba vile wanavyocheza, hawana tofauti na mabeki wengi, naamini watafanya kazi yao ya kuzuia nami nitafanya kazi yangu. Wakae mkao wa kula.”